Michezo

FKF yatangaza ratiba ya raundi ya 16 ya Betway

February 20th, 2020 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

BAADA ya mechi za raundi ya 32 za kuwania ubingwa wa Betway Cup kumalizika, Shirikisho la Soka Kenya (FKF) limetangaza rasmi ratiba ya mechi za raundi ya 16 ambazo zitachezwa Machi 14 na 15.

Katika michuano hiyo, kuna timu za Ligi Kuu (KPL) zitakazokutana, kwa mfano Bandari itakabiliana na Sofapaka wakati Gor Mahia wakivaana na Posta Rangers.

Gor Mahia walifuzu mwishoni mwa wiki, lakini ilibidi wasubiri hadi dakika ya mwisho kupata bao la ushindi kupitia kwa Bonface Omondi ndipo wakaondoka na ushindi wa 3-2 dhidi ya vijana matata wa Naivas, uwanjani MISC Kasarani.

Mechi hii ilikuwa ikielekea kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, lakini Omondi akaokoa Gor dakika ya 92, timu hizo zilipokuwa zimefungana 2-2.

AFC Leopards nao waliibuka na ushindi finyu wa 1-0 dhidi ya makinda wa Elim mjini Kitale katika mechi iliyochezewa Kenyatta Stadium.

Bao hilo muhimu lilifungwa na Elvis Rupia aliyewazidi walinzi wa Elim kabla ya kupachika wavuni kwa kishindo.

Bandari FC ambao ndio mabingwa watetezi walipata ushindi wa 2-0 dhidi ya KSG Ogopa katika mechi iliyochezewa Kenyatta Stadium, Machakos, wafungaji wakiwa Yema Mwana na William Wadri.

Mshindi wa taji hili atawakilisha Kenya katika mashindano ya CAF Confederation Cup msimu ujao.

Mechi za robo-fainali zitachezwa Aprili 11 na 12, huku nusu-fainali ikitarajiwa kufanyika Aprili 9 na 10.

Kinyume na ambavyo imekuwa katika miaka iliyopita, fainali za mwaka huu zitafanyika Mei 30, 2020, ambapo mshindi ataondoka na Sh2 milioni, huku timu ya pili ikipokea Sh1 milioni.

Timu itakayomaliza katika nafasi ya tatu itapewa Sh750,000 ile ya nne ikiweka mfukoni Sh500,000.

Ratiba ya mechi za raundi ya 16 Bora ni: FC Talanta na Kariobangi Sharks, Posta Rangers na Gor Mahia, Sofapaka na Bandari, Bidco United na Fortune Sacco, Keroka Technical na Kisumu All-Stars, Ushuru na AFC Leopards, KCB na Wazito, Migori Youth na Ulinzi Stars.