Michezo

'Flash' afikia rekodi ya Mehta kwenye Safari Rally

March 19th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa Safari Rally mwaka 2004, 2009, 2011 na 2012, Carl ‘Flash’ Tundo amefikia rekodi ya ushindi tano ya mwendazake Shekhar Mehta baada ya kushinda makala ya 66 Jumapili.

Akishirikiana na mwelekezi wake Tim Jessop katika gari la aina ya Mitsubishi Evolution 10, alinyakua taji la tano kwa saa 1:55:05.8.

Mehta, ambaye aliaga dunia mwaka 2006, alishikilia rekodi ya ushindi nyingi za Safari Rally baada ya kutwaa mataji ya mwaka 1973, 1979, 1980, 1981 na 1982.

Bingwa wa Safari Rally mwaka 2013 na 2014 Baldev Chager, ambaye alielekezwa na Ravi Soni katika gari la aina ya Mitsubishi Evolution, aliridhika katika nafasi ya pili (2:04:34.2) naye Mganda Jas Mangat akishirikiana na Joseph Kamya katika gari la aina ya Mitsubishi Evolution akafunga tatu-bora (2:05:27.3).

Makala haya yaliyofanyika siku tatu katika maeneo ya Naivasha kuanzia Machi 16, alivutia madereva 35.

Madereva 22 walikamilisha mashindano, huku bingwa wa Afrika na Kenya mwaka 2015 Jaspreet Chatthe na bingwa wa Afrika mwaka 2017 Manvir Baryan wakiwa katika orodha ya waliojiuzulu kutokana na matatizo mbalimbali.