Michezo

Foden kutia saini mkataba mpya utakaomvunia Sh15 milioni kwa wiki kambini mwa Man-City

November 8th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MWINGEREZA Phil Foden anatarajiwa wiki hii kutia saini mkataba mpya utakaomshuhudia akipokea ujira mpya ambao ni mara tatu zaidi kuliko Sh5 milioni ambao kwa sasa analipwa kwa wiki uwanjani Etihad.

Kocha Pep Guardiola amefichua kwamba usimamizi wa Man-City unaelekea kukamilisha mkataba wa Foden ambaye amejipa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha miamba hao wa soka ya Uingereza.

Foden, 20, aliingia katika sajili rasmi ya Man-City mnamo Julai 2018 na akarasimisha uhamisho wake hadi ugani Etihad kwa mkataba wa miaka sita.

Mbali na kulipwa sasa mshahara wa Sh15 milioni kwa wiki, Foden atakuwa pia na uhakika wa kutia mfukoni marupurupu na bonasi za hadi Sh1.2 milioni kwa kila ushindi utakaokuwa ukisajiliwa na Man-City katika mapambano mbalimbali.

Habari hizo ni nzuri zaidi kwa Foden ambaye ameitwa pia kambini mwa timu ya taifa ya Uingereza licha ya kufurushwa katika kikosi hicho mnamo Septemba kwa kuvunja kanuni za kudhibiti maambukizi ya Covid-19 akiwa na mwenzake Mason Greenwood wa Manchester Uinted.

Huku Greenwood akiachwa nje ya kikosi cha Uingereza, kocha Gareth Southgate atapania zaidi kutegemea huduma za Foden katika mechi zijazo za kimataifa dhidi ya Jamhuri ya Ireland, Ubelgiji na Iceland.