Siasa

Ford Kenya yavuna kutoka kwa DAP-K

May 29th, 2024 2 min read

NA OSBORN MANYENGO

CHAMA cha Ford Kenya tawi la Trans-Nzoia kimepokea wanachama zaidi ya 50 waliohama kutoka DAP-K.

Wanachama hao wakiongozwa na Bw Boaz Werunga ambaye aliwania udiwani wadi ya Tuwani kwa tiketi ya DAP-K kwenye uchaguzi wa mwaka 2022 akashindwa na Francis Were wa ODM, walisema waliamua kurejea nyumbani “baada ya kutambua kwamba chama cha DAP-K hakina mwelekeo hata kidogo”.

Bw Werunga alisema Jumanne jioni kwamba kurejea kwake katika Ford Kenya ni uamuzi wake pamoja na wafuasi wake.

Alisema hakuna yeyote aliyemshinikiza kujiunga na Ford Kenya ila aliona kwamba chama cha Ford Kenya chini ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Masika Wetang’ula ndicho chama kinachomfaa.

“Mimi pamoja na wenzangu hakuna aliyetulazimisha kuingia Ford Kenya bali tuliona heri kuja kwa nyumba iliyo na mpango na imesimama imara kuliko kuwa mahali ambapo hakuna mwelekeo na msimamo,” akasema Bw Werunga.

Aliyewapokea rasmi katika chama ni naibu kinara wa kitaifa wa Ford Kenya ambaye pia ni mbunge wa Kwanza Ferdinand Kevin Wanyonyi.

Bw Wanyonyi aliwataka wote walioingia Ford Kenya kurejea kwa lengo la kuboresha chama.

Alisema chama hicho cha alama ya Simba ni chama kilicho na msingi ikizingatiwa kuwa ni cha cha pili kongwe zaidi nchini baada ya Kanu.

Kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024, mbunge huyo alisema wabunge watakuwa na fursa nzuri ya kuupiga msasa Bunge la Kitaifa litakaporejelea vikao vyake Jumanne juma lijalo.

Bw Wanyonyi alikana madai yanayoibuliwa na baadhi ya wapinzani kwamba wabunge wa nuungano tawala wa Kenya Kwanza wataupitisha mswada huo jinsi ulivyo.

Kuhusu Vuguvugu la Tawe linalopigiwa debe na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, mbunge huyo alimrai kuwazia kujiunga na Ford Kenya na kusitisha mchakato huo wa kusajili Tawe kama chama, akidai kuwa huenda vuguvugu la Tawe Movement likazua uhasama miongoni mwa jamii ya Mulembe.

Kwenye mkutano huo, mbunge huyo aliandamana na viongozi kutoka mashinani ambapo matawi madogo yote matano ya Kaunti ya Trans-Nzoia yaliwakilishwa, akiwemo naibu mwenyekiti wa kitaifa wa Ford Kenya ambaye pia ni diwani maluum Bi Margaret Wanjala.