Habari Mseto

#FormNiGani: Wanaume washirikishwe kupanga uzazi

April 17th, 2018 2 min read

Na CAROLYNE AGOSA

VUGUVUGU moja la kijamii linataka Bunge kutenga bajeti mahususi ya kuimarisha huduma za kupanga uzazi nchini huku idadi ya Wakenya ikigonga 50 milioni.

Vuguvugu hilo linalojitambulisha kwa wito: “FormNiGani”, pia linataka wabunge kuweka mikakati ya kujumuisha wanaume katika kupanga uzazi kwani ni wahusika wakuu katika suala la uzazi.

Wakizungumza Jumanne walipoandaa matembezi katikati ya jiji la Nairobi kuelekea Bunge kuwasilisha hoja yao, wanachama wa vuguvugu hilo walisikitika kwamba mzigo wa kupanga uzazi umeachiwa wanawake.

“Ingekuwa wanaume wanaweza kupata mimba mbinu za kupanga uzazi zingepatikana kwa urahisi zaidi, tena kwa bei nafuu. Hii ni kwa sababu japo mama ndiye hubeba mimba ni wanaume hufanya maamuzi kuhusu idadi ya familia,” akasema mmoja wa waandalizi wa matembezi hayo, Bw George Nderitu.

“Wabunge sasa wanatayarisha bajeti ya mwaka ujao. Tunawahimiza kutenga fedha mahususi ili kuimarisha upatikanaji wa mbinu bora za kupanga uzazi kote nchini, sio kondomu pekee,” aliongeza.

Kampeni hiyo inalenga hususan vijana wenye umri wa miaka kati ya 18-35 limehimiza wanaume kushiriki kikamilifu katika kupanga uzazi.

Wataalamu wanahoji kuwa, mbinu za kupanga uzazi huchangia kuokoa gharama za matibabu kwa akina mama na watoto kwani ni wachache watakumbwa na matatizo ya ujauzito na kujifungua, wala kusaka huduma za kuavya mimba ambazo hawajapangia wala kutarajia.

Ripoti ya Hali ya Uzazi Kenya (KDHS) inaonyesha kuwa karibu nusu ya mimba zote (asilimia 43) huwa hazijapangiwa. Vijana wachanga wa miaka kati ya 15-19 ndio wanaongoza katika kuhitaji huduma za kupanga uzazi.

“Wanawake na wanaume wote wakubaliane idadi na wakati wa kupata watoto.  Vile vile, waandamane kwa kliniki za kupanga uzazi ili wanaume pia wafahamishwe mbinu zinazowafaa angalau pia wasaidie akina mama kubeba mzigo huo,” alieleza Bw Joel Ingo.

Takwimu zaonyesha kuwa mtoto huzaliwa kila sekunde 20 nchini Kenya au 4,237 kwa siku.

Viwango vya uzazi vingali juu huku mwanamke mmoja akitarajiwa kupata watoto 4 maishani mwake.

Kenya itafanya zoezi la kuhesabu watu Agosti mwaka ujao. Zoezi la mwisho mnamo 2009 lilipata idadi ya watu ilikuwa 38,61 milioni.

Makadirio ya kila mwaka yaonyesha idadi hiyo ilipanda hadi 41 milioni mwaka 2011 na imefika 50.95 mwaka huu. Shirika la Umoja wa Mataifa linakadiria kutakuwa na Wakenya 51.7 milioni mwaka 2020.