Makala

Fort Jesus yafunguliwa kufufua utalii Pwani

September 14th, 2020 3 min read

Na DIANA MUTHEU

BAADA ya kufungwa kwa miezi sita sasa, hatimaye kivutio maarufu cha watalii eneo la Pwani, Fort Jesus, ilifunguliwa Jumatatu asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika majengo ya Fort Jesus, mtaalamu wa miundo misingi katika ngome hiyo, Bi Fatma Twahir alisema kuwa eneo hilo sasa limefunguliwa na wamejiandaa vizuri kuwapokea wageni.

Bi Twahir alisema kuwa sehemu za watu kunawa mikono ziko tayari, kwani mifereji na sabuni zimewekwa langoni.

Pia, mtindo wa kulipia tiketi umegeuzwa na malipo yanafanywa kwa njia ya kieletroniki, ambapo wageni wanakubaliwa kutumia M-pesa au kadi za benki pekee.

Zaidi, Bi Twahir alisema kuwa wameweka vidude vya kielektroniki vitakavyotoa viyeyuzi bila kubonyezwa, watu hawaruhusiwi kugusa vitu ovyo ovyo, njia zimewekewa alama ili kuhakikisha wanaotembelea jingo hilo wanasimama umbali wa mita moja unusu, hayo yote kuhakikisha kuwa wageni wako salama na wanalindwa dhidi ya maradhi ya covid-19.

Baadhi ya wageni wakisajiliwa nje ya majengo ya Fort Jesus. Ngome hiyo imefunguliwa leo baada ya kufungwa kwa miezi sita. PICHA/ DIANA MUTHEU

“Baada ya kufunga kwa miezi sita, hatimaye tumefungua na tayari leo tumewapokea wageni karibu 30,” akasema Bi Twahir. Wageni wetu wanapaswa kuvalia barakoa zao, pia tumehakikisha kuwa kuna njia moja itakayofuatwa na wageni wote ili kuhakikisha kuwa watu hawatembei kiholela. Pia, tumeweka ilani kuonyesha idadi ya watu watakaoingia katika vyumba vya maonyesho, ili kuzuia msongamano wa wageni mle ndani,” akasema Bi Twahir.

Pia, mkahawa ulio ndani ya majengo ya Fort Jesus umeagizwa ufuate masharti yaliyowekwa na serikali.

“Tumewaelekeza wafuate mikakati yote iliyopendekezwa na wizara ya Afya, ili kulinda afya yao na ya wateja wao,” akasema Bi Twahir.

Ngome ya Fort Jesus ilifungwa mnamo Machi baada ya kisa cha kwanza cha mgonjwa wa virusi vya corona kutangazwa nchini, pale ambapo makavazi yote nchini yaliamrishwa kusitisha shughuli zao.

Bi Twahir aliiambia Taifa Leo Dijitali kuwa kufungwa kwa makavazi hiyo imekuwa hasara kubwa ikizingatiwa kuwa mapato makubwa hupatikana miezi ya Aprili na Agosti.

Wageni wakitalii ndani ya Fort Jesus, baada ya kivutio hicho cha watalii kufunguliwa. PICHA/ DIANA MUTHEU

“Mwaka jana mnamo Aprili tulipokea wageni 23,000 na mapato ya Sh5 milioni, na mnamo Agosti watalii walikuwa 52,000 huku mapato yakiwa Sh10 milioni. Pia, miezi hiyo ingine tulikuwa tunapata wageni japokuwa hawakuwa wengi,” akasema Bi twahir akiongeza kuwa katika mwezi wa Aprili, shule nyingi zilikuwa zinatembelea makavazi hayo na mwezi wa agosti, wanafunzi watalii wa humu nchini na kutoka nchi za nje walifurika Fort Jesus.

Hata kama mwezi wa Septemba idadi ya wageni wanaotembelea eneo hilo jhuwa wamepungua, Bi Twahir alisema kuwa majengo ya Fort Jesus yako salama na wana matumaini kuwa watapokea watalii wengi.

“Tuna matumaini kuwa wageni wataanza kutembelea eneo hili. Tuko tayari kuwapokea,” akasema afisa huyo.

Bi Twahir alisema kuwa eneo hilo lilikaguliwa na idara ya afya ya umma ya Kaunti ya Mombasa wiki tatu zilizopita, wafanyikazi wote wakapimwa virusi hivyo, na hakuna mmoja aliyeambukizwa maradhi ya Covid-19.

Zaidi alisema kuwa walichukua muda mrefu kujiandaa kupokea wageni, ili kuhakikisha kuwa wamezingatia sheria zote zilizopendekezwa na Wizara ya Afya, na pia kuwafanya wateja wao wawe na Imani na jinsi wanavyotoa huduma zao.

“Rais alipotangaza ufunguzi wa polepole wa uchumi mnamo Juni 2, wafanyikazi wetu walianza kazi za kukarabati na kusafisha eneo lote kwa matayarisho ya kuwapokea wageni. Walifanya kazi kwa kupishana,” akasema.

Watalii wakipigwa picha ndani ya majengo ya Fort Jesus, ilipofunguliwa leo asubuhi. PICHA/ DIANA MUTHEU

Mtalii mmoja kutoka Nairobi, Bw Jacob Simwero alisema kuwa amefurahishwa jinsi mikakati ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona imefuatiliwa katika ngome hiyo.

“Kabla ya kuingia ndani ya Fort Jesus, tuliandikishwa majina, nambari ya simu, tukapimwa joto na ikarekodiwa. Sijawahi kuona sehemu nyingine ambapo kiwango cha joto cha wateja kinanukuliwa. Pia, vidude wanavyotumia kuwekea viyeyuzi inatumia teknolojia ya hali ya juu ambapo hatuhitajiki kugusa pahali popote,” akasema huku akiongeza kuwa anajihisi salama katika mazingira yale na angewaomba Wakenya watembelee makavazi hiyo.

“Nilikuwa nimesoma na kusikia mengi kuhusu Fort Jesus, na mwishowe nimeiona mimi mwenyewe. Sikujua kuwa itafunguliwa leo, nilikuwa katika likizo na nikaamua kupitia eneo hili kuangalia hata angalau jengo lenyewe kwa nje, lakini nashukuru nimeweza kuiona sehemu ya ndani ya ngome hiyo,” akasema Bw Simwero.

Mtembezi wa watalii eneo la Fort Jesus na Old Town, Bw Esgar Gulambasi alisema kuwa janga la corona liliathiri kazi zao, lakini wana matumaini ya kupokea wageni wengi.

Mtaalam wa miundo misingi katika ngome ya Fort Jesus, Fatma Twahir akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangaza kuwa eneo hilo limefunguliwa tena. PICHA/ DIANA MUTHEU

“Maisha yalikuwa magumu. Tulilazimika kufanya kazi mbadala ili kupata fedha za kulisha familia zetu. Tunamwomba Mungu atuondolee janga hili, na atuongezee idadi ya wageni,” akasema Bw Gulabasi huku akiongeza kuwa watu wote wanapaswa kuzingatia sheria zilizowekwa na wizara ya afya, ili kazi ziendelee bila ya maabukizi yeyote ya corona.

Makavazi ya Fort Jesus, fuo za bahari za umma kama vile Jomo Kenyatta maarufu ‘Pirates’ na bustani za kujivinjari kama vile Mama Ngina ni baadhi ya maeneo yaliyofungwa punde tu kisa cha kwanza cha mgonjwa wa maradhi ya covid-19 kutangazwa.

Fort Jesus ndilo jengo zee zaidi katika eneo la Pwani, kulingana na historia. Jengo hilo linaaminiwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 400.

Ni mojawapo ya vivutio vya utalii ambacho huvutia wageni wengi zaidi katika ukanda wa Pwani na jumuiya ya Afrika Mashariki, na siku hizi ni makavazi ya kuhifadhi vyombo vya kale, michoro na miundo mbalimbali ya zana za kivita.