Michezo

Fowadi 'Crucial' Wasambo kurejea KPL

September 18th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAADA ya kupona jeraha la kifundo cha mguu ambalo lilimweka nje kwa msimu mzima uliopita, chipukizi wa Harambee Stars U-20, Vincent Wasambo sasa anatafuta hifadhi mpya baada ya kuagana na Kariobangi Sharks.

“Kwa sasa sina mkataba na Sharks ila ninawaniwa na vikosi kadhaa ambavyo vimenipokeza ofa ninazozitathmini kabla ya kufanya maamuzi,” akasema winga huyo.

Wasambo almaarufu ‘Crucial’ alikuwa ameanza kuwa tegemeo kuu kambini mwa Sharks chini ya kocha William Muluya hadi alipopata jeraha baya lililomweka nje kwa mwaka mzima wa 2019.

Baada ya kupona, sasa chipukizi huyo amefichua azma ya kurejea ugani kwa matao ya juu akivalia mojawapo ya vikosi vya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) vinavyomezea mate huduma zake.

“Nashukuru Sharks kwa kusimama nami katika kipindi kizima cha kuuguza jeraha ambalo nusura litamatishe ghafla taaluma yangu ya usogora. Sasa nimepona na napania kurejelea mazoezi mazito nikipiga hesabu kuhusu kikosi cha kujiunga nacho,” akasema Wasambo.

Sharks ambao kwa sasa wako chini ya kapteni Eric Juma, wamerejelea mazoezi katika uwanja wa Utalii Grounds.

Mabingwa hao wa SportPesa Super Cup tayari wameagana na nyota Sven Yidah aliyeyoyomea Nairobi City Stars na wamepanga kufichua silaha zao mpya kwa minajili ya msimu ujao wa 2020-21 wikendi hii.