Michezo

Fowadi John Avire wa Harambee Stars atua Aswan SC nchini Misri

December 1st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Aswan SC kimemsajili fowadi wa Harambee Stars, John Avire, kwa mkataba wa miaka miwili kutoka Tanta SC ambao ni wapinzani wao wakuu katika Ligi ya Misri.

Avire aliingia katika sajili rasmi ya Tanta mnamo Agosti 2019 baada ya kuagana na Sofapaka almaarufu ‘Batoto ba Mungu’ waliotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mnamo 2009.

Akivalia jezi za Tanta almaarufu ‘The Yellows’, alicheka na nyavu za wapinzani wao mara moja pekee kutokana na mechi 10 na akashindwa kuzuia waajiri wake kushushwa ngazi kwenye Ligi Kuu katika msimu wa 2019-20.

Tanta SC ilianzishwa mnamo 1926 na ni miongoni mwa klabu kongwe zaidi barani Afrika.

Kwa kuingia kambini mwa Aswan, anakuwa mchezaji wa 21 kusajiliwa na kikosi hicho ambacho kimejinasia mseto wa wanasoka wazoefu na idadi kubwa ya chipukizi kwa minajili ya kampeni za msimu huu. Miongoni mwa wachezaji wapevu waliotua Aswan muhula huu ni Ahmed ‘Okka’ Said na Ahmed Salem safi.

Avire, 23, anakuwa mwanasoka wa kutoka nje ya Misri kusajiliwa na Aswan ambao pia wamejitwalia maarifa ya Omar Al-Dahi wa Yemen na Mohammad Balah ambaye ni raia wa Nigeria.

Utajiri wa kipaji cha Avire katika ulingo wa soka ni jambo lililompa nafasi ya kuwa miongoni mwa washambuliaji tegemeo kambini mwa Harambee Stars kwenye kikosi kilichoshiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri. Alikuwa sehemu ya kikosi cha Stars kilichopiga Tanzania 3-2 kabla ya kupepetwa 3-0 na Senegal kwenye hatua ya makundi.

Kwa upande wao, Sofapaka wameapa kuanzisha mchakato wa kisheria kuzuia uhamisho wa Avire ambaye kwa mujibu wa rais wa kikosi hicho, Elly Kalekwa, aliyoyomea Misri mwishoni mwa 2019 kuvalia jezi za Tanta kinyume na kanuni za usajili zilizopo katika mwongozo wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).