Michezo

Fowadi McGoldrick wa Sheffield United na timu ya Jamhuri ya Ireland astaafu soka ya kimataifa

November 6th, 2020 1 min read

Na MASHARIKI

MSHAMBULIAJI David McGoldrick wa Sheffield United amestaafu rasmi soka ya kimataifa baada ya kuchezea timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland jumla ya michuano 14 pekee.

Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Ireland (FAI) limesema kwamba sogora huyo mwenye umri wa miaka 32 McGoldrick aliangika rasmi daluga zake ili kumakinikia soka ya kiwango cha klabu na kuyazamia majukumu ya familia.

Mchuano wa kwanza ambao nyota huyo alicheza akivalia jezi za Jamhuri ya Ireland ni kivumbi kilichowakutanisha na Amerika mnamo 2014.

McGoldrick alifunga bao lake la pekee ndani ya jezi za timu ya taifa mnamo 2019 katika sare ya 1-1 dhidi ya Uswisi.

McGoldrick alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka katika kikosi cha kwanza cha Jamhuri ya Ireland mnamo Agosti 2020.

“FAI inampongeza McGoldrick kwa kujitolea kwake na kila mara alipochezea timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland. Amekuwa kielelezo chema kwa chipukizi wengi kikosini na tunamtakia kila la heri katika soka ambayo kwa sasa analenga kumakinikia katika ngazi ya ligi,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Ireland.