Fowadi Moise Kean awabeba PSG hadi ndani ya 32-bora French Cup

Fowadi Moise Kean awabeba PSG hadi ndani ya 32-bora French Cup

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) walifuzu kwa hatua ya 32-bora ya French Cup msimu huu baada ya kupiga Caen ya Ligi ya Daraja la Pili katika soka ya Ufaransa 1-0 mnamo Jumatano.

PSG wametawazwa mabingwa wa taji la French Cup mara tano katika kipindi cha misimu sita iliyopita.

Fowadi Moise Kean anayechezea PSG kwa mkopo kutoka Everton ndiye alifungia kikosi cha kocha Mauricio Pochettino bao hilo la pekee na la ushindi dhidi ya Caen. Goli hilo lilikuwa la 12 kwa Kean kupachika wavuni hadi kufikia sasa msimu huu.

Licha ya ushindi, kitakachomkosesha usingizai kocha Pochettino ni jeraha alilolipata fowadi tegemeo wa PSG, Neymar Jr mwishoni mwa kipindi cha kwanza dhidi ya Caen.

PSG kwa sasa wanatazamiwa kuwaalika Barcelona kwa mchuano wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Februari 16, 2021 uwanjani Parc des Princes, Ufaransa.

Ni mechi itakayorejesha kumbukumbu za 2017 ambapo PSG walikung’uta Barcelona 4-0 katika mkondo wa kwanza jijini Paris kabla ya Barcelona kulipiza kisasi na kuwabandua miamba hao wa Ufaransa kwa ushindi mnono wa 6-1 kwenye marudiano yaliyofanyika uwanjani Camp Nou nchini Uhispania.

AS Monaco, Marseille na viongozi wa jedwali la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), Lille pia walifuzu kwa hatua ya 32-bora ya French Cup baada ya kuibuka washindi wa mechi zao mnamo Jumatano usiku.

Marseille walipepepta Auxerre 2-0, Lille wakapokeza Dijon kichapo cha 1-0 nao Monaco wakasajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Grenoble.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Iheanacho atokea benchi na kuokoa chombo cha Leicester City...

Azidi kumiminiwa sifa kwa kutumia talanta yake katika...