Michezo

Fowadi Thuram wa Borussia Monchengladbach aonyeshwa kadi nyekundu kwa kumtemea mpinzani mate usoni

December 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIUNGO mvamizi Marcus Thuram wa Borussia Monchengladbach alionyeshwa kadi nyekundu kwa hatia ya kumtemea mate usoni beki Stefan Posch wa Hoffenheim wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mnamo Disemba 19, 2020.

Monchengladbach walipoteza mechi hiyo kwa mabao 2-1.

Thuram, 23, alionyeshwa kadi nyekundu moja kwa moja katika dakika ya 79 baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba alidhihirisha utovu wa nidhamu kwa kumtemea mate beki Posch ambaye ni raia wa Austria.

Tukio hilo lilifanyika dakika chache baada ya Andrej Kramaric kusawazishia Hoffenheim waliokuwa wakichezea ugenini.

Nyota wa Tottenham Hotspur anayechezea Hoffenheim kwa mkopo, Ryan Sessegnon alifunga bao la ushindi katika dakika ya 86.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Thuram ambaye ni mtoto wa Lilian Thuram aliyeongoza Ufaransa kushinda Kombe la Dunia mnamo 1998 kuonyeshwa kadi nyekundu tangu aanze kuvalia jezi za Monchengladbach kwenye Bundesliga misimu miwili iliyopita.

M’gladbach ambao watacheza na Manchester City katika hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), sasa wanashikilia nafasi ya nane jedwalini na hawajashinda mechi yoyote kati ya sita zilizopita katika mashindano yote. Kwa upande wao, Hoffenheim wanashikilia nafasi ya 11 jedwalini.