Michezo

Fowadi wa Harambee Stars Paul Were atia saini mkataba mpya kambini mwa PAE Eagaleo nchini Ugiriki

September 24th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI wa Harambee Stars, Paul Were amerefusha mkataba wake kwa mwaka mmoja zaidi katika kikosi cha PAE Egaleo kinachoshiriki Ligi ya Daraja la Tatu nchini Ugiriki.

“Tuna furaha kutangaza kwamba Paul Were amerefusha kandarasi yake kambini mwetu kwa miezi 12 ijayo,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Egaleo.

Kwa upande wake, Were alisema: “Egaleo ni kikosi ambacho kimenihifadh vyema. Kwa hakika nilikuwa na ofa nyingi za kujiunga na klabu nyinginezo. Lakini ofa zao hazikuwa zinakaribiana kivyovyote na ile ya Egaleo.”

“Bado nina kibarua ambacho napania kukikamilisha kambini mwa Egaleo na kubwa zaidi katika matamanio yangu ni kuongoza kikosi hiki kupanda daraja kwenye ligi,” akaongeza Were.

“Nina kiu ya kuendeleza ubabe niliojivunia kabla ya kuja kwa janga la corona na tuna kila sababu ya kujikweza pazuri mwishoni mwa msimu huu,” akasema.

Egaleo walipepetana na Asteras Tripolis ya Ligi Kuu ya Ugiriki kirafiki mnamo Septemba 24, 2020. Mechi hiyo ilichezewa ndani ya uwanja mtupu bila mashabiki.

Mnamo Januari 29, 2010, Were alijiunga na Tusker kutoka Mathare Youth. Alihudumu kambini mwa kikosi hicho kwa misimu miwili na nusu na kuongoza miamba hao kutwaa taji la Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Nyota huyo aliingia katika sajili rasmi ya AFC Leopards mnamo Juni 6, 2012.

Mnamo Februari, 10, 2014, alitua Afrika Kusini kushiriki majaribio na kikosi cha Bidvest Wits kabla ya kusajiliwa na AmaZulu mnao Julai 16, 2014.

Kushushwa ngazi kwa kikosi hicho kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) kulishuhudia Were akiagana na AmaZulu mnamo Juni 2015 baada ya msimu mmoja pekee.

Aliingia kambini mwa Kalloni FC nchini Ugiriki mnamo Agosti 20, 2015 kisha kusajiliwa na Denizilspor FC ya Uturuki kwa mkataba wa mwaka mmoja mnamo Agosti 7, 2016.

Were alichezeshwa kwa mara ya kwanza kambini mwa Harambee Stars mnamo Februari 9, 2011 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Afrika Kusini.