Habari Mseto

France 24 yaungana na Signet kufaidi wenye runinga za dijitali

March 29th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

SHIRIKA la Habari la Kimataifa la France 24 limetia saini makubaliano na mawimbi ya Signet ili kupeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kiingereza kupitia runinga za dijitali.

Makubaliano hayo yataiwezesha chombo hicho cha habari kufikia zaidi wakenya 2.3 milioni hapa nchini.

Japo wamedumu humu nchini tangu mwaka wa 2009 shirika hilo limekuwa likipeperusha matangazo yake kwa Kiswahili kupitia Radio France International katika miji ya Mombasa na Nairobi kupitia mawimbi ya FM.

“Tumekuja Kenya siyo kwa sababu tunalenga biashara au kutoa ushindani kwa vyombo vingine vya habari. Lengo letu ni ni kufikia watazamaji wengi na kuwajulisha kuhusu matokeo yote duniani,” akasema Mkurugenzi Mkuu Jean-Emmanuel Casalta anayesimamia mikakati na maendeleo katika shirika hilo.

Hata hivyo alisisitiza kwamba chombo hicho kipya kitashirikiana na vyombo vya habari vya nyumbani katika maswala muhimu yanayoathiri jamii na nchi kwa jumla.

“Sisi hatutapiginia nafasi ya kupeperusha matangazo ya kibiashara kwa kuwa nia yetu si kufaidi kifedha ila tutaangazia mambo ibuka yanayoathiri jamii na taifa hili,” akasema.

Afisa huyo pia alisisitiza kwamba kwa kuanzisha televisheni hiyo kwa lugha ya kingereza wanalenga kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na mataifa ya Magharibi mwa Afrika ambako lugha ya kifaransa huzungumzwa mno.

Kwa sasa France 24 inapatikana kupitia Zuku, Azam, Starsat na satelaiti za NSS 12 na SES 5. Inapeperusha habari zake katika zaidi ya nchi 150 na inakadaria watazamaji wake kutoka bara la Afrika huwa 29 milioni.

Lugha za Kiarabu, Kihispania, Kifaransa pia hutumika kupeperusha matangazo ya shirika hilo ambalo lina wanahabari 430 kote duniani.