Michezo

Frank de Boer apokezwa mikoba ya timu ya taifa ya Uholanzi

September 24th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA wa zamani wa Ajax, Frank de Boer ameteuliwa kuwa mkufunzi wa timu ya taifa ya Uholanzi.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 amepokezwa mkataba wa miaka miwili ambao utatamatika mwishoni mwa fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa nchini Qatar mnamo 2022.

Kuteuliwa kwa beki huyo wa zamani wa Ajax na Barcelona kunachochewa na haja ya kujaza pengo la ukufunzi lililoachwa na Ronald Koeman aliyepokezwa mikoba ya Barcelona mnamo Agosti 2020 baada ya Quique Setien kutimuliwa kwa matokeo duni ugani Camp Nou.

De Boer aliwahi kuwajibishwa katika jumla ya mechi 112 akivalia jezi za Ajax, Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi.

Amewahi pia kuwatia makali vijana wa Inter Milan nchini Italia, Crystal Palace nchini Uingereza na Atlanta United katika Major League Soccer (MLS) nchini Amerika kati ya Disemba 2018 na Julai 2020.

De Boer ndiye alikuwa kocha msaidizi wa Uholanzi kikosi hicho kilipotinga fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini chini ya ukufunzi wa Bert van Marwijk.

Akiwanoa Ajax kati ya Disemba 2020 na Mei 2016, De Boer aliongoza kikosi hicho kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya Uholanzi.

Mchuano wa kwanza kwa De Boer kusimamia kambini mwa Uholanzi ni ule wa kirafiki utakaowakutanisha na Mexico jijini Amsterdam mnamo Oktoba 7, 2020 kabla ya kuwaongoza vijana wake kuvaana na Bosnia-Herzegovina na Italia katika UEFA Nations League mnamo Oktoba 11 na Oktoba 14, 2020 mtawalia.