Michezo

Fred sasa ni kidume kamili, afunga bao la hakika

February 4th, 2019 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO wa Manchester United, Fred sasa ameingia kundi la majanadume kamili baada ya mchuma wake Monique Salum kumzalia mtoto wa kiume kwa jina Benjamin.

Sogora huyo mzawa wa Brazil, 25, alifunga orodha ya wanasoka wa Man-United waliojaliwa vimalaika mwishoni mwa Februari.

Awali, Nemanja Matic, Paul Pogba na Romelu Lukaku wote walivuka mwezi wa Januari vyema baada ya refa wa mahaba kuyahesabu mabao waliyoyafunga dhidi ya wake na wachumba wao mnamo 2018.

“Karibu sana duniani Benjamin, fahari ya familia yangu na Monique,” Fred aliandika kwenye mtandao wake wa Instagram huku akipakia picha za awali za ujauzito wa mkewe.

Uhusiano kati ya Fred na Monique ulifichuka kwa mara ya kwanza mnamo Januari 2016 wawili hao walipoonekana pamoja wakiponda raha jijini Donetsk, Ukraine.

Ilikuwa hadi Februari mwaka jana ambapo kiungo huyo wa zamani wa Shakhtar Donetsk alipomvisha demu wake pete ya uchumba.

Kwa sasa Victor Lindelof na Matteo Darmian ndio wachezaji wengine wa Man-United wanaotarajia wake zao kuwazalia watoto. Darmian anatarajia refa wa mahaba kulihesabu bao lake kwa mkewe Francesca Cormanni mwishoni mwa Machi huku Maja Nilsson akitazamia kumkopolea Lindelof mtoto wa kiume wakati wowote mwezi huu.