Habari Mseto

Fujo chuoni baada ya mwanafunzi kuuawa

February 11th, 2018 2 min read

 

Jengo la klabu ya Dalawa mjini Bondo ambalo lilichomwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST) Februari 10, 2018 baada ya mwenzao wa mwaka wa tatu kuuawa Ijumaa usiku. Picha/ Justus Ochieng

Na JUSTUS OCHIENG

Kwa Muhtasari:

  • Mauaji ya mwanafunzi yachochea maandamano makubwa, huku wanafunzi wakichoma klabu mjini Bondo
  • Mwanafunzi huyo alidungwa kisu cha mauti wakati wa mapigano mwendo wa saa nane za usiku
  • Steve Owino Otombo, alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu, aliyekuwa akisomea kilimo

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga kilichoko kaunti Siaya aliuawa kwa kudungwa kisu kwenye mgogoro katika baa moja usiku wa kuamkia Jumamosi.

Mauaji hayo yaliibua maandamano makubwa, ambapo wanafunzi wa chuo hicho walichoma klabu hicho mjini Bondo.

Kulingana na Naibu Chansela wa chuo hicho Prof Stephen Agong, baadhi ya wanafunzi kutoka chuoni humo walianza kupigana na wahudumu wa baa hiyo mjini Bondo. Ni wakati huo ambapo mwanafunzi wa mwaka wa tatu alidungwa kwa kisu.

“Wanafunzi walizozana na wahudumu wa baa katika kisa ambacho kinachunguzwa na polisi. Taarifa tuliyo nayo ni kwamba mwanafunzi wetu alidungwa kisu na kufa wakati wa makabiliano hayo,” akasema Prof Agong.

Kamishna wa Kaunti ya Siaya anayeondoka, Bi Josephine Onunga, alisema mwanafunzi huyo alidungwa wakati wa mapigano mwendo wa saa nane za usiku.

“Alikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Bondo ambamo aliaga dunia,” alisema Bi Onunga.

Jengo la klabu ya Dalawa mjini Bondo ambalo lilichomwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST) Februari 10, 2018 baada ya mwenzao wa mwaka wa tatu kuuawa Ijumaa usiku. Picha/ Justus Ochieng

Prof Agong’ alisema polisi Bondo wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho.

“Hili ni suala la polisi na tayari wameanzisha uchunguzi. Tutatoa habari zaidi baadaye, ni wazi kwamba hayo yalikuwa mauaji,” alisema Naibu Chansela.

Marehemu, Steve Owino Otombo, alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu, aliyekuwa akisomea kilimo.

Aliuawa baada ya mashindano ya DJ katika klabu ya Dala-wa kugeuka mapigano.

Naibu Kamishna wa Kaunti Bondo Richard Ojwang’ alisema mambo yaligeuka wakati baadhi ya wanafunzi walihisi walikuwa karibu kupoteza katika mashindano hayo.

Wanafunzi hao walizua rabsha, na ni wakati huo ambapo mwanafunzi huyo alidungwa kwa kisu.

“Wanafunzi hao walitoka nje ili kulalamika kabla ya kuanza kurusha mawe, hali iliyozua mapigano,” alisema Bw Ojwang’.

Makabiliano makali yalizuka kati ya wanafunzi na wakazi, na ndipo mwanafunzi huyo alipodungwa.