Kimataifa

Fujo msanii stadi akizikwa

July 2nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

ADDIS ABABA, ETHIOPIA

MWANAMUZIKI maarufu nchini Ethiopia, Hachalu Hundessa ambaye aliuawa akiliendesha gari lake, jana alizikwa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama.

Kifo cha msanii huyo mnamo Jumatatu katika hali ya kutatanisha kilizua maandamano makubwa nchini Ethiopia na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.

Hata hivyo, sababu ya kuuawa kwake bado hazijulikani japo mwenyewe aliwahi kusema hadharani kuwa amepokea jumbe za kumtishia maisha kutoka kwa watu asiowafahamu.

Kulingana na kituo cha runinga kinachomilikiwa na serikali cha EBC, zaidi ya watu 81 wameuawa kutokana na makabiliano kati ya raia na polisi hasa katika eneo la Oromia tangu kifo cha Hundessa.

Marehemu Hundessa amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali kupitia nyimbo zake na ametajwa kati ya waliopigania mageuzi yaliyosababisha mabadiliko ya utawala mnamo 2018.

Waandamanaji wenye hasira mnamo Jumatano walivamia mji mkuu wa Addis Ababa huku milipuko mitatu ya bomu ikiripotiwa jijini humo.

Huku mazishi hayo yakiendelea nyumbani kwake katika mji wa Ambo, polisi walitoa taarifa kwamba watu watatu wanaotuhumiwa kuhusika katika kifo chake tayari wamenyakwa na uchunguzi unaendelezwa na kitengo hicho.

Mauaji ya mwimbaji huyo yamepandisha taharuki nchini Ethiopia ambayo hivi majuzi iliahirisha uchaguzi wake wa wabunge na urais, ikitaja kuchipuka kwa virusi vya corona kama sababu kuu ya kutoandaliwa kwa kura hiyo.

Taharuki imepanda jijini Addis Ababa mnamo Alhamisi huku baadhi ya wakazi wakijikusanya na kuunda makundi ili kulinda biashara na mali yao kutoka kwa makundi ya vijana wenye hasira wanaolalamikia kifo cha Hundessa.

Barabara za mji wa Addis Ababa mchana wote Alhamisi zilikuwa mahame huku magari na malori yaliyoteketezwa na waandamanaji yakionekana katika baadhi ya barabara za mji huo.

Huduma za intaneti na data bado hazijarejeshwa nchini Ethiopia huku makundi ya kutetea haki za kibinadamu yakilalamika kuwa hiyo ni njama ya serikali ya kuficha ukweli kuhusu idadi ya watu waliouawa.

“Kuzimwa kwa mitandao kumeifanya iwe vigumu kupata habari kuhusu waliouawa na wale waliojerujiwa wakati wa maandamano ya kulalamikia mauaji ya Hundessa,” akasema afisa mmoja wa kundi la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch.

Kati ya walionyakwa wiki hii ni mtetezi maarufu wa haki za kibinadamu Jawar Mohammed na zaidi ya wafuasi wake 30. Hata hivyo, kunyakwa kwa viongozi wa upinzani pia kumezidisha joto la kisiasa nchini Ethiopia na kuongeza wimbi la maasi linaloendeshwa na wafuasi wao.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliyeingia uongozini mnamo 2018 baada ya maandamano ya kung’oa utawala uliokwepo wakati huo, amelaumiwa kwa kukandamiza uhuru wa kujieleza miongoni mwa raia.

Aidha, baadhi ya mabadiliko ya kisiasa ambayo utawala wake umekuwa ukiyatekeleza, umekuwa ukipingwa na kudaiwa kuzidisha migawanyiko ya kikabila na mapigano yanayoishia kwenye maafa.

Abiy ametaja mauaji ya msaani huyo kama ‘janga’ na kusema ‘maadui’ wa utawala wake hawatafanikiwa kutatiza uongozi wake.