Habari

Fujo nyumbani kwa Ruto

October 9th, 2019 2 min read

Na CECIL ODONGO na CHARLES WASONGA

VIJANA wenye hasira kutoka eneobunge la Kibra, walizua rabsha Jumanne wakitaka kuingia nyumbani kwa Naibu Rais William Ruto katika mtaa wa Karen, Nairobi.

Vijana hao walilalamikia kufungiwa nje ya mkutano ulioandaliwa katika makao hayo rasmi ya Naibu Rais kupanga mikakati ya jamii ya Abagusii kumuunga mkono Bw McDonald Mariga wa chama cha Jubilee kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra utakaofanyika Novemba 2019.

Viongozi wa jamii ya Abagusii wakiongozwa na Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi na wabunge wanane, walihudhuria mkutano huo uliofanyika Jumanne asubuhi.

Mbunge wa Mugirango Kusini, Sylvanus Osoro alidai fujo hizo zilisababishwa na watu ambao si wa jamii ya Abagusii.

“Kila aliyefaa kuhudhuria mkutano huo alitumiwa ujumbe kwa sababu tulipanga ziara hiyo kupitia makundi ya jamii yetu Wakisii. Walioalikwa walikuwa wameketi kwenye hema kufikia saa moja asubuhi na walikuwa watu 5,000 wa kabila letu wanaoishi Kibra,” akasema Bw Osoro.

Mbunge huyo wa Chama cha Kenya National Congress (KNC) alisema waliokuwa nje walitarajia kwamba wangehutubiwa na Naibu Rais baada ya kikao hicho, lakini hilo halikufanyika ndiposa wakazua rabsha nje ya makazi hayo.

“Matukio hayo ni kawaida Kibra na sisi Wakisii hatujawahi kushiriki vituko hivyo. Wale ambao huwa na tabia hiyo wanajulikana wazi,” akasema Bw Osoro.

Bw Maangi naye alisema waliozua fujo hawakuwa wamealikwa.

“Mimi ninafahamu kwamba tuliwaalika watu na waliokuwa nje hawangeruhusiwa kwa kuwa mkutano ulikuwa ukiendelea na viongozi walikuwa wameanza kuhutubu. Tunashauri jamii yetu inayoishi Kibra kumuunga mkono Bw Mariga hapo Novemba 7,” akasema Bw Maangi.

Dkt Ruto amekuwa akiandaa vikao vya kisiasa katika makao hayo ya Karen kwa kualika wajumbe kutoka jamii mbalimbali zinazoishi Kibra.

Jamii ya Waluo

Leo Jumatano inatarajiwa wajumbe kutoka jamii ya Waluo wanaoishi Kibra watakutana naye kumdhihirishia kwamba wanamuunga mkono Bw Mariga.

Huku hayo yakijiri, wabunge wa chama cha ODM wameibua madai kwamba kuna njama ya kuvuruga sajili ya wapigakura ya Kibra.

Kwenye kikao cha Jumanne na wanahabari katika majengo ya bunge, wabunge hao walisema leo wataenda katika afisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuitisha sajili ya wapigakura itakayotumika katika uchaguzi huo mdogo.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi na Mkurugenzi wa uchaguzi Junet Mohamed, walisema ni wajibu wa IEBC kutoa sajili kwa wadau wote katika uchaguzi huo.

Anayepeperusha bendera ya ODM katika uchaguzi huo mdogo ni kakake aliyekuwa Mbunge wa eneo bunge hilo marehemu Ken Okoth, Imran Okoth. Atakapambana na Bw Mariga (Jubilee), Eliud Owalo (ANC), Khamisi Butichi (Ford Kenya) miongoni mwa wengine.

Mwishoni mwa wiki, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi aliitaka serikali kuchunguza madai kuwa kuna watu wanaonunua vitambulisho vya kitaifa katika eneo bunge hilo la Kibra kwa lengo ya kuwanyima wapigakura haki ya kushiriki uchaguzi huo.