Michezo

Fulham wakaba Liverpool koo na kuwanyima fursa ya kutua kileleni mwa jedwali la EPL

December 14th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) walipoteza fursa ya kupaa hadi kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 na Fulham mnamo Disemba 13, 2020 uwanjani Craven Cottage.

Mohamed Salah aliwavunia Liverpool alama moja katika mchuano huo kupitia penalti ya dakika ya 79 baada ya Aboubakar Kamara kuunawa mpira wa ikabu uliochanjwa na kiungo Georginio Wijnaldum.

Bobby Decordova-Reid aliwaweka Fulham uongozini katika dakika ya 25 na kikosi hicho cha kocha Scott Parker kingalifunga mabao mengine matatu katika kipindi cha kwanza iwapo kipa Alisson Becker angalizembea katikati ya michuma.

Mlinda-lango huyo raia wa Brazil, alifanya kazi ya ziada na kuzipangua fataki alizoelekezewa na Ivan Cavaleiro aliyewatatiza pakubwa mabeki wa Liverpool.

Liverpool waliponea pia kuadhibiwa baada ya refa Anre Marriner kulazimika kutazama mtambao wa VAR ili kubaini iwapo tukio lililomshuhudia Fabinho akimkabili Cavaleiro ndani ya kijisanduku lilistahili kuwapa Fulham penalti.

Zaidi ya kupoteza alama mbili muhimu, pigo zaidi kwa Liverpool ya kocha Jurgen Klopp katika mechi hiyo ni jeraha alilolipata beki Joel Matip ambaye kwa sasa anajiunga na orodha ndefu ya wanasoka wanaouguza majeraha kambini mwa miamba hao wa soka ya Uingereza.

Kati ya wachezaji hao Virgil van Dijk, Joe Gomez, Trent Alexander-Arnold, Thiago Alcantara, James Milner, Naby Keita, Xherdan Shaqiri na Diogo Jota.

Makombora yaliyoelekezwa na Jordan Henderson, Salah na Sadio Mane langoni mwa Fulham yalidhibitiwa kirahisi na kipa Alphonse Areola.

Liverpool walitarajiwa kuchuma nafuu na kutia kibondoni alama zote tatu muhimu katika mechi hiyo baada ya Chelsea na Tottenham Hotspur ambao ni wapinzani wao wakuu ligini msimu huu kupoteza pointi muhimu wikendi.

Spurs ya kocha Jose Mourinho ililazimishiwa sare ya 1-1 na Crystal Palace uwanjani Selhurst Park mnamo Disemba 13, siku moja baada ya Everton kuwazamisha Chelsea kwa 1-0 uwanjani Goodison Park.

Liverpool kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 25 sawa na viongozi Spurs. Leicester City waliwapepeta Brighton 3-0 mnamo Disemba 13 uwanjani King Power na kupaa hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 24, moja zaidi kuliko nambari nne Southampton.