Fulham wawika ugenini na kuendeleza masaibu ya Liverpool katika EPL msimu huu

Fulham wawika ugenini na kuendeleza masaibu ya Liverpool katika EPL msimu huu

Na MASHIRIKA

MASAIBU ya Liverpool katika kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu yaliendelezwa na Fulham mnamo Jumamosi baada ya kupokezwa kichapo cha 1-0 uwanjani Anfield.

Huku ushindi wa Fulham ukiweka hai matumaini yao ya kusalia ligini msimu ujao, kichapo ambacho masogora wa kocha Jurgen Klopp walipokezwa kilididimiza zaidi matumaini yao ya kumaliza kampeni za muhula huu ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2021-22.

Bao la pekee na la ushindi ambalo Fulham walipata katika gozi hilo lilipachikwa wavuni na Mario Lemina – fowadi raia wa Gabon anayechezea kikosi hicho cha kocha Scott Parker kwa mkopo kutoka Southampton.

Alama tatu ambazo Fulham walitia kapuni ziliwadumisha katika nafasi ya 18 kwa alama 26 sawa na nambari 17, Brighton. Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Fulham kujivunia uwanjani Anfield tangu 2012.

Liverpool walinyanyua taji la EPL msimu uliopita wa 2019-20 wakijivunia pengo la alama 18 kati yao na nambari mbili Manchester City. Hadi Liverpool walipopigwa na Burnley mnamo Januari 2021, miamba hao wa soka ya Uingereza hawakuwa wamepoteza mechi yoyote ya nyumbani kutokana na mapambano 68 ya EPL.

Hivyo, kichapo kutoka kwa Fulham kilikuwa cha sita mfululizo kwa Liverpool kupokea baada ya chombo chao kuzamishwa na Brighton, Manchester City, Everton na Chelsea hapo awali kwa usanjari huo.

Klopp alikifanyia kikosi alichokitegemea dhidi ya Chelsea mabadiliko manane muhimu alipowaongoza Liverpool kuchuana na Fulham waliomtatiza pakubwa kipa Allison Becker kupitia mafowadi Ademola Lookman na Josh Maja.

Mechi hiyo ilimpa Klopp fursa ya kumwajibisha fowadi Diogo Jota kwa mara ya kwanza tangu Novemba 28, 2020. Ingawa alishirikiana vilivyo na Sadio Mane na Mohamed Salah, nyota huyo wa zamani wa Wolves alishuhudia makombora yake yakidhibitiwa vilivyo na kipa Alphonse Areola.

Liverpool ambao kwa sasa hawajashinda mchuano wowote kati yam inane iliyopita, wanajivunia alama 43, nne nyuma ya Chelsea wanaofunga mduara wa nne-bora.

Liverpool ndicho kikosi cha kwanza kuwahi kupoteza jumla ya mechi sita mfululizo za EPL katika uwanja wao wa nyumbani baada ya Huddersfield Town mnamo Februari 2019.

Fulham ndicho kikosi cha kwanza limbukeni katika EPL kuwahi kushinda Liverpool katika EPL uwanjani Anfield tangu Blackpool waongozwe na kocha Roy Hodgson kufanya hivyo mnamo Oktoba 2010.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kurudiana na RB Leipzig ya Ujerumani katika hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo Machi 10, 2021. Wataingia ugani kwa minajili ya mechi hiyo jijini Budapest, Hungary wakijivunia ushindi wa 2-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza.

Kwa upande wao, Fulham wana wiki nzima ya kujiandaa kuchuana na viongozi wa jedwali la EPL, Manchester City waliopigwa 2-0 na Man-United katika mechi nyingine ya Jumapili.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Moi ndiye mrithi wa Uhuru, Kanu yasema

UDA yaelekeza macho yake 2022 baada ya London