Michezo

Fulham yazamisha Leicester 2-1 katika EPL na kuachia wengine kuburura mkia

December 1st, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Scott Parker wa Fulham alimtunuka sifa fowadi Ivan Cavaleiro baada ya penalti ya nyota huyo kusaidia kikosi chake kuangusha Leicester City na kujiondoa kwenye orodha ya vikosi vilivyopo katika hatari ya kushushwa ngazi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Hadi mkwaju wa Cavaleiro ulipotikisa nyavu za Leicester, kikosi cha Fulham kilikuwa kimepoteza penalti tatu za awali kwa mfululizo. Kushindwa kwa Leicester kulinyima Leicester ya kocha Brendan Rodgers nafasi ya kutua kileleni mwa jedwali la EPL na kufikia Tottenham Hotspur.

Cavaleiro ambaye ni raia wa Ureno, alikuwa pia amepoteza penalti ya awali katika ushindi wa 3-2 uliosajiliwa na Everton dhidi yao mnamo Novemba 22, 2020 uwanjani Craven Cottage.

Aleksandar Mitrovic aliwahi pia kupoteza penalti dhidi ya Sheffield United mnamo Oktoba kabla ya Ademola Lookman kupoteza nyingine katika mchuano wa EPL uliowakutanisha Fulham na West Ham United mnamo Novemba 7, 2020.

Wakicheza dhidi ya Leicester, Lookman aliwaweka Fulham uongozini katika dakika ya 30 baada ya kumwacha hoi kipa Kasper Schmeichel. Bao hilo lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Andre-Frank Zambo Anguissa.

Cavaleiro alifanya mambo kuwa 2-0 katika dakika ya 38 kupitia penalti iliyotokana na hatua ya beki Christian Fuchs kumchezea Bobby Decordova visivyo.

Awali, Leicester walikuwa wameshuhudia makombora yao mawili yaliyopigwa na Wesley Fofana na Youri Tielemans yakigonga mwamba wa goli la Fulham. Ilikuwa hadi dakika ya 86 ambapo Harvey Barnes aliyetokea benchi katika kipindi cha pili aliposawazishia Leicester.

Ushindi wa Fulham ambao ni wao wa pili hadi kufikia sasa msimu huu, uliwakweza hadi nafasi ya 17 jedwalini kwa alama saba, sita zaidi kuliko Sheffield United wanaovuta mkia.

Kwa upande wao, Leicester walisalia katika nafasi ya nne kwa alama 18, tatu nyuma ya viongozi Tottenham na Liverpool.

Lookman ambaye anachezea Fulham kwa mkopo kutoka RB Leipzig ya Ujerumani, alisherehekea bao lake dhidi ya Leicester kwa kuinua jezi ya kiungo wa zamani wa Senegal, Papa Bouba Diop aliyeaga dunia mnamo Novemba 29 akiwa na umri wa miaka 42.

Baada ya kuvaana sasa na Zory Luhansk ya Ukraine kwenye Europa League mnamo Disemba 3, Leicester wameratibiwa kuchuana na Sheffield United ugani Bramall Lane mnamo Disemba 6, 2020. Kwa upande wao, Fulham wana siku nne zaidi za kupumzika kabla ya kuwaendea Manchester City kwa gozi la EPL mnamo Disemba 5, 2020 ugani Etihad.