Fuliza: Ruto sasa aokoa mahasla riba ikipungua

Fuliza: Ruto sasa aokoa mahasla riba ikipungua

NA WINNIE ONYANDO

NI afueni kwa Wakenya wanaotegemea mkopo wa simu wa Fuliza baada ya kampuni ya Safaricom ikishirikiana na serikali ya Rais William Ruto kupunguza riba kwa asilimia 50 kuanzia Oktoba.

Rais Ruto alisema hatua hiyo inanuia kuwainua wafanyabiashara wadogo wadogo wanaotegemea mikopo kama hiyo.Rais alisema kuwa kupunguzwa kwa riba kutawasaidia Wakenya kuchukua mkopo kuendesha shughuli zao za kibiashara, jambo analosema litainua uchumi wa nchi.

“Haya ni maendeleo chanya kwa kuwa mamilioni ya Wakenya ambao wanategemea mikopo wataweza kuendeleza shughuli zao. Tutaendelea kushirikiana na kampuni za fedha ili kupunguza zaidi riba ya mikopo,” akasema Rais Ruto.

Kwa upande mwingine, Rais alitoa wito kwa Wakenya kukopa ikiwa kuna hitaji.

“Unafaa kukopa kuinua biashara au kuwekeza. Hata hivyo, tunawahimiza Wakenya kuweka akiba,” akasema Rais Ruto.

Kwa upande mwingine, alisema serikali itawekeza katika kuwainua vijana na wafanyabiashara ndogo ndogo kama vile mama mboga kupitia ‘hustler fund’.

Rais alisema kuwa Wakenya milioni nne watatolewa kwenye orodha ya CRB inayohusisha waliochelewa au kukosa kulipa mikopo yao, mwanzoni mwa mwezi wa Novemba.

“Kuna Wakenya wengi ambao wamekwama CRB kwa kushindwa kulipa madeni. Hata hivyo, kuanzia mwezi wa Novemba, hao wote watatolewa,” akasema Dkt Ruto.

Aliahidi kuwa serikali yake itaweka mikakati ya kubadili mtindo wa kuwaweka Wakenya CRB.

Kwa upande wake, mkurugenzi Mkuu wa Safaricom, Bw Peter Ndegwa, alisema hatua hiyo ni kuwapunguzia mzigo Wakenya wanaotegemea aina hiyo ya mkopo.

Hivyo, wateja wanaochukua kati ya Sh101 hadi Sh500 na mikopo kati ya Sh501 hadi Sh1,000 watatozwa riba ya asilimia sita kwa siku.Kwa hiyo, mikopo ya hadi Sh1,000 itapunguzwa riba kutoka Sh10 hadi Sh6.

Wateja watakaochukua mkopo kati ya Sh1,001 hadi Sh1,50O watapunguziwa kwa asilimia 10 huku wale wanaokopa kati ya Sh1,501 na Sh2,500 watafurahia punguzo la asilimia 20.

Watumiaji wa Fuliza wanaokopa kati ya Sh2,501 hadi Sh70,000 watapunguziwa riba kwa asilimia 16.7.

Naye mkuu wa NCBA, Bw John Gachora, alisema zaidi ya Wakenya 28 milioni wanatumia Fuliza tangu izinduliwe mwaka wa 2019.Bw Gachora aliahidi kuwa watatatua suala la CRB ifikapo Novemba.

Kadhalika, alisema kupunguzwa kwa riba ya Fuliza ni hatua ya kwanza tu ya juhudi za kufanya mikopo kuwa nafuu kwa wateja.

Fuliza huwawezesha watumiaji wa M-PESA kuendeleza biashara zao hata kama hawana fedha za kutosha katika akaunti yao ya M-PESA.

Kadhalika, wateja pia watapata muda wa siku tatu kabla ya kuanza kulipa mikopo yao.

Fuliza ilizinduliwa Januari 5, 2019, kwa ushirikiano na Benki ya Biashara ya Afrika.

  • Tags

You can share this post!

Namwamba aahidi kufufua sekta ya michezo nchini

Kenya kuandaa handiboli ya Zone 5 ya U18 na U20 Oktoba

T L