Habari Mseto

Fuliza sasa yabisha kwa soko la kimataifa

March 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Safaricom imetangaza mpango wa kueneza huduma yake mpya ya Fuliza, itumiayo M-Pesa, kwa mataifa sita Afrika.

Kampuni hiyo inalenga kuimarisha mapato yake kupitia kwa huduma hiyo ya mkopo papo hapo.

Mataifa yanayolengwa ni Tanzania, Lesotho, Ghana, DRC, na Mozambique ambako huduma ya M-Pesa inaendelea kupitia kwa kampuni ya Vodacom.

Vodacom imeweza pia kutoa huduma za M-Pesa India. Huduma ya Fuliza huwasaidia watumiaji wa M-Pesa kukopa mikopo ya kiwango kidogo na kuilipa katika muda mfupi.

Wateja wanaweza kupata kufikia Sh70,000 kwa mkupuo kulipia bidhaa na huduma.

Huduma hiyo ilizinduliwa Januari na Safaricom ikishirikiana na Commercial Bank of Africa (CBA) na KCB.

Huduma hiyo inaweza pia kupatikana na watumiaji wa laini zingine zisizo za Safaricom.

“Tumetathmini Fuliza katika mataifa mengine iliko Vodacom. Kuna mataifa saba Afrika ambayo hutumia M-Pesa na tunalenga kupeleka Fuliza humo kwanza,” alisema Afisa wa Fedha wa Safaricom Sitoyo Lopokoiyit.

Kulingana naye, Safaricom inalenga kueneza huduma zake na bidhaa nje ya Kenya.

Watumiaji wa M-Pesa Tanzania, DRC, Mozambique na Lesotho waliongezeka kwa wateja 227,000 katika muda wa miezi mitatu hadi 13.4 milioni kufikia Desemba mwaka jana kulingana na Vodacom.

Nchini Kenya, watumiaji wa M-Pesa ni milioni 21 na idadi inaendelea kuongezeka.