Habari Mseto

'Fuliza' yatua TZ

July 24th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

KAMPUNI ya mawasiliano kutoka Tanzania, Vodacom, imeanza kuwapa wateja wake huduma za kutuma pesa ama kufanya manunuzi kwa simu hata wasipokuwa na pesa za kutosha, sawa na huduma zinazotolewa Kenya na Safaricom kwa jina ‘Fuliza’.

Huduma hiyo ambayo imepewa jina ‘Songesha’ nchini humo sasa itawawezesha watumizi wa laini za kampuni ya Vodacom, ambayo ina uhusiano na Safaricom ya Kenya kukamilisha huduma za M-Pesa hata wasipokuwa na pesa za kutosha kwenye simu.

Kulingana na huduma hizo, mteja anaweza kupewa deni la kiwango fulani kulingana na jinsi amekuwa akitumia huduma za M-Pesa, mkopo ambao utalipiwa riba ya asilimia 1 ndani ya siku 18.

“Tumeshirikiana na benki ya TPB ili kuwezesha huduma hizi. Benki ndiyyo itafanya hesabu kubaini mtu anaweza kupewa kiwango gani cha mkopo huo,” akasema Mkurugenzi wa Biashara wa Vodacom Tanzania Epimack Mbeteni.

Huduma hiyo imeanzishwa Tanzania baada ya kuanzishwa nchini Kenya Januari, ikivutia watumizi milioni 4.2 kwa kipindi cha mwezi, hali iliyoonyesha uhitaji mkubwa wa mikopo ya haraka katika uchumi.

Kutokana na kukua kwake kwa kasi, kampuni ya Safaricom ilitangaza mpango wa kuieneza huduma hiyo kwa mataifa mengine sita, yakiwemo Tanzania, Lesotho, Ghana, DR Congo na Msumbiji.

Ili kuwezesha huduma hiyo, kampuni ya mawasiliano inashirikiana na benki, ambayo huwapa watumizi wa M-Pesa mikopo ya kujazia pesa wanazokosa, wakati wanapotaka kutuma pesa ama kununua kitu kutumia M-Pesa.

Kulingana na kampuni ya Vodacom, watumizi wa M-Pesa Tanzania, DR Congo, Msumbiji na Lesotho waliongezeka kufikia milioni 13.4 Desemba 2018, mapato yake pia yakipanda.

Safaricom ilisema kuwa iliamua kuanzisha huduma ya Fuliza baada ya kugundua kuwa mamilioni ya watu kila siku walikuwa wakifutilia huduma za kununua kitu ama kutuma pesa, kwa kukosa pesa za kutosha katika simu.