HabariSiasa

Fundi adai Sh195 milioni za kiti kilichokaliwa na Mzee Moi akiwa rais

June 11th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI huenda ikalipa mamilioni ya pesa kusuluhisha nje ya mahakama kesi kuhusu kiti kilichokaliwa na Rais mstaafu Daniel Moi, ambacho ilirudisha kwa kampuni iliyokitengeneza miaka 26 iliyopita.

Mnamo Februari 2018, serikali iliambia mahakama kwamba haitaki kuendelea na kesi iliyoshtakiwa na kampuni ya Furncon Limited kupitia mkurugenzi wake Solomon Njoroge Kiore.

Kampuni hiyo ilishtaki serikali 2007 kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa kukataa kuilipa baada ya kusanifu, kutengeneza na kupeleka viti viwili vya kukaliwa na rais kulingana na zabuni iliyokuwa imeshinda 1992.

Ikiomba mahakama iruhusiwe kusuluhisha kesi nje ya mahakama, serikali ilitaja suala hilo kuwa tata.

Bw Kiore anasema hatua ya serikali ya kukataa kulipia viti hivyo ilizamisha biashara yake kwani hawezi kutumia karakana ambayo viti hivyo vimehifadhiwa.

“Ni kiti cha mamlaka ya rais. Kilitumiwa na Rais kwa mwaka mmoja. Ni kifaa kinachoheshimiwa na kwa hivyo hakuna anayeruhusiwa kukishika. Biashara yangu imeharibika kabisa kwa sababu ya kiti hiki. Siwezi kuruhusu yeyote kuchezea kiti cha mamlaka ya rais,” anaeleza Bw Kiore.

Ametenga iliyokuwa karakana yake na kuiita “Makao ya Kiti cha Rais.” Kiti hicho kimefungiwa kwenye kasha linalofunikwa kwa bendera ya Kenya ndani ya jengo lililokuwa karakana yake.

Alipowasilisha kesi 2007, alikuwa akitaka mahakama iagize serikali imlipe Sh195 milioni lakini huenda pesa hizo zikaongezeka akitoza ada ya kuhifadhi kiti hicho kwa miaka 26.

Anasema japo serikali haikuwa imewasiliana naye tangu Februari 27, 2018 ilipoomba muda wa kusuluhisha kesi nje ya korti, ana matumaini kiti hicho kitakuwa moja ya turathi zitakazohifadhiwa katika maktaba ya makavazi ya ikulu iliyobuniwa majuzi.

Bw Kiore hakupinga ombi la serikali la kusuluhisha kesi nje ya mahakama ishara kwamba anataka isuluhishwe kwa amani.

Haikuwa mara yake ya kwanza kusanifu na kuuzia serikali samani za kutumiwa katika hafla za kitaifa.

Anasema alitengeneza viti hivyo chini ya usimamizi mkali wa jeshi na maafisa kutoka Ikulu.

Kwenye kesi yake, anasema kampuni yake ilishinda zabuni iliyotangazwa na Idara ya Ulinzi (DoD) na baadaye ikaidhinishwa na Ikulu.

Kampuni iliombwa kutengeneza viti zaidi vya kutumiwa na rais katika ikulu ndogo na kambi za kijeshi.

Inasema shida ilianza ilipoagizwa kupeleka viti katika ofisi za maonyesho ya kilimo ya Nairobi kwa hafla ya siku tatu iliyohudhuriwa na rais.

Kulingana na barua ambayo ASK ilimwandikia Agosti 5 1999, Rais Moi aliagiza viti hivyo vihifadhiwe katika ofisi hizo.

Hivi ndivyo viti ambavyo vilisababisha kesi ambayo sasa serikali inataka kusuluhisha nje ya korti.