Makala

FUNGUKA: ‘Amenigeuza ngoma ila nampenda kupindukia’

February 14th, 2018 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

Kwa Muhtasari:

  • Huenda binti huyu akavunja rekodi kwa kuongoza orodha ya vipusa walioleweshwa na kupumbazwa na penzi
  • Japo binti huyu kabarikiwa na urembo na kiakili, hana bahati katika masuala ya mahaba
  • Nilipomhoji mume wangu, alinishambulia kwa mangumi na mateke, kitendo kilichoniacha na majeraha mabaya
  • Marafiki zangu wamefanya kila wawezalo kunitenganisha naye lakini kwangu penzi hili hatari ni sumaku

UNAPOPATA  fursa ya kusikia hadithi ya Miriam, 30, hauna shaka ila kuamini waliyosema wahenga kuwa kipendacho roho hula nyama mbichi.

Huenda binti huyu ambaye ni mhudumu wa kiafya katika mojawapo ya hospitali kuu eneo la Nakuru akavunja rekodi kwa kuongoza orodha ya vipusa walioleweshwa, kuduwazwa na hata kupumbazwa na penzi.

Kwanza kabisa hebu nikupe maelezo mafupi kumhusu. Alizaliwa mtoto wa nne katika familia yao eneo la bonde la ufa ambapo tangu utotoni alikuwa aking’aa kimasomo.

Kwa bahati mbaya hakufaulu kupata alama za kutosha kumwezesha kusomea udaktari, lakini kutokana na penzi lake la masuala ya matibabu akaamua kusomea uuguzi.

 

Donge nono

Baada ya kukamilisha kozi yake chuoni, binti huyu alibahatika kupata ajira katika mojawapo ya hospitali zinazotambulika ambapo huu ukiwa mwaka wake wa sita katika kazi hii, ni miongoni wa wahudumu wa kiafya wanaoheshimika na kupokea donge nono katika hospitali hiyo.

Isitoshe, uzuri wake kisura na kimaumbile umemfanya kuwa kivutio cha wanaume wengi hasa anakofanya kazi.

Lakini japo binti huyu kabarikiwa na urembo na akili, hana bahati katika masuala ya mahaba. Bibi huyu amenasa jicho la kaka fulani ambaye ni mwanajeshi ambapo wamekuwa wachumba kwa miaka mitano sasa.

Kinachofanya uhusiano wao usiwe wa kawaida ni kwamba miaka michache iliyopita binti huyu aligundua kuwa dume hili lilikuwa na mke na watoto ambao lilikuwa limewaficha eneo la mashambani.

 

Mangumi na mateke

“Niligundua kupitia simu niliyopokea kutoka kwa mwanamke aliyejitambulisha kama mkewe, akiniarifu kuwa kaka huyu ni mumewe na baba ya wanawe watatu.

Nilipomhoji mume wangu, alinishambulia kwa mangumi na mateke, kitendo kilichoniacha na majeraha mabaya kiasi cha kunifanya kulazwa hospitalini kwa mwezi mmoja.

Na pigo hili limekuwa kama ada kila ninapomuuliza kuhusu mkewe ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu nilipogundua.

Kwa mfano nakumbuka wakati mmoja alinipiga vibaya na kunivunja miguu, hatua iliyoaniacha nikitumia kiti cha magurudumu kwa mwezi mmoja. Kadhalika kuna wakati ambapo alinipiga na kunifanya nipoteze mimba ya miezi mitatu, vile vile kupoteza fahamu kwa wiki mbili.

 

Kichapo chageuka sumaku

Lakini la kushangaza ni kuwa muda unavyozidi kusonga ndivyo ninavyozidi kumpenda mwanamume huyu huku kichapo chake kikiwa sumaku kwake. Baada ya kupona majeraha ninayoyapata mikononi mwake, mimi mwenyewe ndiye humtafuta.

Kisa hicho cha mwisho ambapo nilipoteza mimba, mambo yalikuwa mabaya sana kiasi cha kuwa ndugu yangu alipiga ripoti polisi na kuhakikisha kwamba ametiwa nguvuni. Lakini ni mimi mwenyewe niliyemlipia dhamana na kumuondoa jela na kukataa kumshtaki mahakamani.

Jamaa na hata marafiki zangu wamefanya kila wawezalo kunitenganisha naye lakini kwangu penzi hili hatari ni sumaku ambapo sawa na ndimu inavyoongeza ladha kwenye uji, linazidi kunoga kila ninapopokea kichapo”.