FUNGUKA: ‘Dume kivuruge namba wani…!’

FUNGUKA: ‘Dume kivuruge namba wani…!’

Na PAULINE ONGAJI

WANAPOHOJIWA kuhusu sifa za mwanamume bora, kwa wanawake wengi, ukorofi hauwezi ukajumuishwa kwenye orodha yao.

Ukweli ni kwamba wanawake wengi huenzi amani katika mahusiano na nyumbani na kamwe hawawezi kumstahimili mwanamume mkorofi tena jeuri.

Lakini kwake Kate, mambo ni tofauti sana. Yeye anavutiwa sana na madume jeuri na wasio na nidhamu.

Kate ana umri wa miaka 37 na kimasomo ameneemika. Kwa sasa anasomea shahada ya uzamifu katika chuo fulani hapa nchini. Kitaaluma pia kafanikiwa kwelikweli. Yeye ni mkurugenzi wa shirika moja lisilo la kiserikali.

Hajaolewa licha ya kuchumbiwa na madume kadhaa watanashati na wa haiba ya juu. Inasemekana kwamba kizingiti kikuu ni masharti yake yasiyo ya kawaida inapowadia wakati wa kuwachagua wapenzi. Kwake, ukorofi na ujeuri ndivyo vivutio vyake kama anavyoeleza mwenyewe.

“Napenda mwanamume mkorofi na jeuri ajabu, ambaye mbali na kuwa na mazoea ya kunikosea heshima kila mara kupitia ukorofi na matusi yake, pia anaweza kuniporomoshea mangumi akijiskia.

Mwanamume mlevi ajabu ambaye akishakunywa vya kwake, anatusi watu klabuni na hata kuzua vurugu. Dume linalonilaghai kimapenzi kwa kuwa na mahusiano kadha wa kadha ya pembeni.

Nafurahia mwanamume ambaye haoni haya ya kurusha mbegu zake huku na kule. Ninaposema hivi namaanisha kwamba, mwanamume aliyewazalisha wanawake kadhaa huko nje.

Kwangu, ujeuri na ukorofi ni vivutio na vichocheo vya penzi hata zaidi. Kwangu, mwanamume mpole na mtiifu anachosha na ni dhaifu katika ulimwengu wangu.

Kwa hivyo mojawapo ya sifa ninazotafuta ninapomsaka mpenzi, ni kaka mwenye mwili mkubwa zaidi kuniliko. Nikisema mwili mkubwa namaanisha kwamba dume la kimo kirefu, vile vile mnene.

Kupitia mwili wake mkubwa, basi itakuwa rahisi kwake kunipiga wakati wowote ule, na pia kusababisha vurugu kila mara na hata kunitandika.

Kitabia, lazima awe kivuruge, sio mwanamume mtiifu na mwenye heshima. Dume ambalo liko tayari kupinga na kukiuka maagizo yangu.

Lazima kaka anoe kinywa chake na kujifunza kurusha mvua ya maneno makali kila mara.

Chumbani sharti anipandishe ashiki kwa lugha chafu ya kunikosea heshima.

Niko tayari kumkubali kaka asiye na sifa hizi, lakini mradi tu ataahidi kubadilika na kukubaliana na matakwa yangu tunavyozidi kusonga mbele katika uhusiano.

Masharti yangu haya yamefanya iwe changamoto kumpata mwenzi kwani kila ninapovitaja vigezo hivi, wengi hutoweka. Kwa wale ambao hukubali, muda unavyozidi kusonga, wao pia hutoroka na wakidhani mimi ni mwenda-wazimu.

Lakini japo masharti haya yamechangia pakubwa ugumu wa kudumisha uhusiano, silegezi kamba kamwe, na kwa yeyote anayetamani kuwa mpenzi, mchumba au mume wangu katika siku zijazo, basi itambidi kukubaliana na matakwa yangu”.

You can share this post!

Nyong’o aondoa hofu kuhusu corona inayoshuhudiwa India

CHOCHEO: Usimkaribie tu, mguseguse…