FUNGUKA: ‘Haja yangu pesa tu!’

FUNGUKA: ‘Haja yangu pesa tu!’

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA mazingira haya magumu ya kiuchumi, harusi imekuwa shughuli ghali kwa wengi ambapo ni wachache walio na uwezo wa kumudu gharama za sherehe hii bila usaidizi kutoka kwa jamaa na marafiki.

Ni sababu ambayo imefanya wengi kujitosa katika michango kila inapowadia wakati huu, ili kukusanya pesa kufanikisha shughuli hii.

Lakini japo wengine hutumia jukwaa hili vyema, kwa Karol, hii imekuwa mbinu ya kuwahadaa na kuwapokonya mali madume.

Karol ni binti wa umri wa miaka 36 na mama wa watoto wawili. Kimasomo, amejikakamua na kujifadhili kielimu hadi chuo kikuu ambapo ana shahada yake ya uzamili.

Kitaaluma pia yupo ngangari. Katika kipindi cha miaka kumi, binti huyu amepanda madaraka katika shirika analofanya kazi na kufikia wadhifa wa usimamizi.

Kimaumbile pia, kaneemeka. Kutoka nywele, ngozi yake nyororo, hadi umbo lake la kipekee, kwa kweli Maulana aligonga ndipo alipokuwa akimuumba.

Lakini kando na uzuri huu, ana tabia nyingine ya kiajabu. Karol ana mazoea ya kuwahadaa wanaume kwamba watafunga ndoa, kabla ya kuwashawishi kuandaa mipango ya kuchangisha pesa, ila pindi fedha zinapokusanywa, hutoweka bila hata kwaheri. Na hana aibu kukusimulia hilo.

“Kutokana na uzuri wangu, kwa kawaida mimi huwa na msururu wa madume wanaoniandama wakitaka kunioa, ambapo niliona hii kuwa fursa nzuri ya kujinufaisha.

Kabla ya kukukubali, lazima nifanye utafiti kuhusu kaka ninayelenga. Kwanza kabisa sharti dume liwe tajiri na lina mwunganisho wa marafiki wa haiba ya juu.

Kwa nini nasisitiza kuhusu mwunganisho wa aina hii? Hilo litanipa jukwaa murwa kukusanya kitita kikubwa cha fedha kutoka kwao. Aidha, litaniwezesha kupata windo langu la mradi ufuatao.

Pindi nikitambua kwamba nimevuta jicho la kaka fulani, nitafanya uchunguzi kuhakikisha kwamba ana sifa zote ninazotaka.

Kisha nitamnasa na kumpagawisha kwa mapenzi moto moto hadi aamini keshapata. Nitamsukuma kunitambulisha kwa jamaa na marafiki zake na kuhakikisha anajulikana kwetu pia nikilenga posa na mahari.

Baadaye tutaanza kupanga harusi ambapo mimi huhakikisha dume linaniamini kabisa kiasi cha kunipa mamlaka ya kusimamia masuala ya pesa.

Kumaanisha shughuli zote za sherehe kutoka kwa nguo ya Bi harusi, mapambo, magari yatakayohusika, hadi sehemu ambapo maankuli yataandaliwa, ni mimi nitashika usukani.

Hatimaye huanza kuchangisha pesa na hata ikichukua mwaka mzima kupata kiwango tunachohitaji, sitapoteza subira. Pindi kiwango hicho kinapopatikana, basi nitamuagiza mweka hazina kunipa pesa zote ili kuanza maandalizi ya harusi.

Nikishapokea, nitaibua kijisababu cha kuliacha dume. Mara kadhaa nimetumia mabinti wanaowanasa hao akina kaka na kuwashawishi kushiriki mahaba nao. Kisha katika shughuli hiyo, lazima wapige picha na kunitumia. Picha hizi zinakuwa ushahidi tosha wa kuliacha dume bila maswali.

Kufikia sasa nimewahadaa wanaume sita na niko katika harakati za kulinasa windo langu la saba”.

You can share this post!

Obiri kuongoza Kenya kuhifadhi dhahabu ya Olimpiki mita...

CHOCHEO: Usiwe mwepesi wa kumeza chambo