Makala

FUNGUKA: 'Hana mali, amejaza vimada ila nampenda'

March 7th, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

WANASEMA kwamba penzi kikohozi na hakuna ambaye anasawiri msemo huu vyema kama Irene.

Kwa wanawake wengi na hasa wale ambao wamewahi kuwa na wapenzi au hata kuolewa watakuambia kwamba hakuna kitu wanachodhibiti kama himaya yao, ambapo hakuna ambaye yuko tayari kuacha apokonywe hivi hivi.

Lakini kwa binti huyu mambo ni tofauti kabisa ambapo uvumilivu wake ni wa viwango vya kipekee. Kwanza kabisa wacha nikupe taarifa fupi kumhusu.

Irene ana miaka 37 na ni mama wa watoto wawili wavulana; miaka 15 na miaka 10.

Yeye ni mfanyabiashara ambapo ana duka la kuuza malazi viungani mwa jiji la Nairobi. Maisha ya Irene kamwe hayajakuwa rahisi kwani mumewe alimuacha wanawe wakiwa wangali wadogo na kwenda kuoa sio mke mmoja, bali wawili.

Kabla ya hatimaye kumuacha, kaka huyu alikuwa amebobea kwa dharau. Kwa mfano, wakati huo alikuwa akimletea Irene wanawake wengine nyumbani na kwa chumba chao na hata kushiriki mahaba nao mbele ya binti huyu.

Wakati huu wote, dume hili lilikuwa limetelekeza majukumu yake kama mwanamume huku likimuachia Irene wajibu wa kukidhi mahitaji ya wana wao. Kumbuka wakati huo, walikuwa na mali ikiwa ni pamoja na vilabu viungani mwa jiji, na magari kadhaa.

Lilipomuacha binti huyu, halikumuachia chochote ila jukumu la kukidhi mahitaji ya watoto wao. Hata hivyo, baada ya kuishiwa, hatimaye mwaka jana dume hili liliamua kumrejelea binti huyu, na hata liliporudi halikuacha hao wanawake wengine.

Bila shaka watu walimtarajia Irene kudinda kumkubali, lakini mambo hayakuwa hivyo.

“Naam, aliniomba nirudi lakini ombi lake kuu lilikuwa nikubali wale wanawake wawili wengine wawe wake wenza. Ni suala ambalo sikufikiria hata mara mbili ila nilikubali licha ya jamaa zangu kulipinga vikali.

Nimemruhusu arejee kwani bado ananitambua sio tu kama mkewe, bali bibi wa kwanza. Hao wawili wako lakini wanafahamu kwamba mimi ndiye niliyewatangulia na hivyo sharti waniheshimu.

Hata hivi majuzi tulikuwa kijijini ambapo alikuwa amempoteza nyanyake. Kwenye matanga alituambia sisi sote watatu tufike. Na katika mkutano na jamaa zake aliulizwa ni yupi kati yetu anayempenda ambapo alikiri penzi lake kwetu sote. Hata hivyo alinitaja kama mke wa kwanza na kwangu hiyo inatosha.

Na sio kwamba ana mali. Yeye amerejea lakini bado mimi lazima nifanye biashara yangu kukidhi mahitaji yangu na wanangu. Lakini, mradi anashughulikia mahitaji yetu sote kimahaba basi sina tatizo.

Namkubali kwani yeye ndiye baba ya wanangu na naamini sana umuhimu wa kudumisha familia. Hata jamaa zangu na hasa mamangu amekuwa akinishauri kwamba niolewe na mtu mwingine lakini siwezi.

Marafiki wanadhani kwamba nimepagawa wakisema kwamba uhusiano wa aina hii unatuweka katika hatari ya kupata maradhi ya zinaa na hasa virusi vya HIV.

Hata hivyo, mimi sina tatizo kwani najua kwamba tunaaminiana, na najua kwamba mume wangu ana uwezo wa kuwadhibiti hao wake zake wengine sawa na anavyonifanyia.”