Makala

FUNGUKA: ‘Hata na hiki kitambi, sukari ya warembo naramba’

September 5th, 2020 2 min read

NA PAULINE ONGAJI 

Lewis ni mwanamume wa miaka 45. Kwa viwango vya kawaida, kuna baadhi ya watu ambao kidogo watasita kumuorodhesha miongoni mwa madume watanashati.

Ana kimo cha futi tano na kitambi kilichochomoza, suala linalomfanya kuonekana mfupi hata zaidi.

Ana kichwa kidogo cha mviringo, ngozi inayokwaruza na pia kimavazi sio stadi, kwani ana mazoea ya kuvalia nguo zilizompweya.

Lakini ni udhaifu ambao huenda ameusawazisha kwa mfuko wake mzito. Kwa zaidi ya mwongo mmoja, Lewis amekuwa akifanya kazi na mashirika ya kimataifa, huku mara nyingi ajira yake ikimpeleka katika mataifa ya kigeni kama vile Afghanistan, Somalia na Sudan Kusini.

Na katika harakati hizo, amewekeza ambapo amejenga majumba ya kupangisha mjini Mombasa.

Mkewe na wanawe wanaishi maisha ya starehe kwani hawakosi chochote. Bwana huyu ana mke na watoto wawili ambao wako katika shule ya upili. Lakini licha ya kuwa na familia, ni stadi wa mahusiano ya pembeni.

Kutokana na sababu kuwa mara nyingi hayuko nchini, amepiga nakshi ujuzi wake wa kuvizia mabinti hasa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Yeye ni muongo ajabu ambapo licha ya kuwa kavishwa pete na mkewe, kwa njia moja au nyingine, amefanikiwa kuwanasa mabinti kila anaporusha chambo mtandaoni, kiasi cha kupanga deti haraka upesi, kama anavyosimulia.

“Na ninapozungumzia mabinti, simaanishi kwamba wale vipusa wa kawaida wanaonaswa mtandaoni kiholela. La!

Ni mabinti wanaojielewa; vipusa walio na taaluma za kuheshimika.Mara nyingi tunapokutana mtandaoni, nahakikisha kwamba nawamiminia sifa na ahadi tele.

Hii ni mbinu mwafaka ya kuhakikisha kwamba wanajawa na penzi kwangu hata kabla ya tukutane na kwamba pindi tutakapokutana, hawataweza kuniacha licha ya kutoridhishwa na uzuri wangu kimaumbile.Wanapouliza kuhusu pete iliyo kidoleni, mara nyingi huwajibu mimi na mke wangu tumeachana na kwamba pete hiyo imesalia kidoleni mwangu ili kuwafurusha mabinti wanaoniandama.

Miongoni mwa hao wanawake niliofanikiwa kuwaingiza mtegoni, nimepangia wanne nyumba katika nchi tofauti.Pengine unajiuliza nawadhibiti vipi?

Nina nambari tofauti za simu ambapo kila mwanamke maishani anajua moja tu.Nazima nambari zingine za simu nikiwa na mwanamke mmoja, na hivyo kuondoa shaka inayotokana na simu na jumbe kutoka kwa wanawake wengine kumiminika.

Naweza zima simu hata kwa wiki mbili.Kati ya wanawake hawa- ikiwa ni pamoja na mke wangu, hakuna hata mmoja ambaye ni rafiki yangu kwenye mtandao wa Facebook.

Nikiwa na mwanamke tofauti, hutonipata mtandaoni, kumaanisha kwamba wengine hao hawawezi nifikia.

Nyakati zingine ikinibidi kuwa mtandaoni, nahakikisha kwamba natumia usiri wa hali ya juu.

Kuna baadhi ya watu wanaoniuliza kwa nini nafanya hivi? Na huwajibu kwamba najua hakuna kati yao anayenipendanna badala yake wanataka kunufaika tu kutokana na mfuko wangu. Kwa hivyo hata mimi nawakanganya”.