Makala

FUNGUKA: Lengo langu ni kupata zaidi ya watoto 9

June 27th, 2018 2 min read

NA PAULINE ONGAJI

Katika umri wa miaka 34 kuna wanawake ambao huenda hata hawajafanya uamuzi wa iwapo wako tayari kuolewa au kupata watoto.

Lakini kwa Prisca, katika umri huu tayari anahesabu mwanawe wa tisa huku nia yake ikiwa ni kuwa akitimu miaka 45, atakuwa amepata mtoto na madume kutoka robo ya idadi ya kaunti nchini.

Huku wanawe wakiwa kati ya umri wa miaka 4 na 17, kinachoshangaza hata zaidi ni kuwa licha ya kudondoa hao watoto wote, kisura huyu yungali mrembo ajabu huku umbo lake likiwa thabiti kiasi cha kuvutia macho ya wengi kila anapopita.

Kufikia sasa amefanikiwa kuzaa na madume kutoka Kaunti za Nairobi, Kiambu, Machakos, Kajiado, Vihiga, Kakamega, Mombasa, Kisumu, Busia na Nyamira.

Kutokana na kuwa binti huyu ni msomi na ana taaluma nzuri, suala la fedha halimkoseshi usingizi kwani mshahara anaopata unamwezesha kukidhi mahitaji ya watoto hawa. Kwa hivyo nini hasa kinachomsukuma binti mrembo na anayejisimamia kifedha kutaka kuishi maisha ya aina hii?

“Nataka fahari ya kuwa na mtoto kutoka kila sehemu nchini, lakini bila shaka hilo siwezi afikia. Ndiposa najikakamua angaa kuafikia asilimia 25 ya ndoto yangu katika upande huu. Tangu zamani nimekuwa nikitamani kuonja dume kutoka kila sehemu nchini na hili ni jaribio.

Kadhalika ningependa kuchanganya sifa zangu za kipekee na mbegu kutoka sehemu mbalimbali nchini kama mbinu ya kufanya utafiti nitakaotumia kushauri mabinti zangu wakikomaa kuhusu ni wapi wanapaswa kuolewa.

Pesa sio kigezo muhimu cha kuchagua iwapo unataka kuwa baba wa mwanangu, lakini nimebahatika kupata madume wenye mifuko mizito kila ninapochagua.

Ni hiari yako kuchangia pesa za matumizi za mwanao lakini usinitarajie kukufuata kwani mimi mwenyewe nina pesa zangu. Lakini sharti utie saini mkataba kuwa japo utamsaidia mwanao, hakuna siku hata moja utajitokeza kumtaka.

Kufikia sasa siwezi lalama kwani baba za watoto hao wote hunipa pesa za matumizi kila mwezi.

Baadhi ya mambo muhimu ambayo mimi huzingatia kabla nimchague kaka ni akili ya kipekee ambapo sharti uonyeshe werevu wako kimasomo na kitaaluma. Usafi pia ni jambo muhimu kwani sitaki jeni za uchafu kupitishwa kwa wanangu.

Kadhalika sharti uwe tayari kukubali kuwa baada ya kupanda mbegu hakutakuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi ndiposa haijalishi iwapo umeoa au la.

Baba wote wa wanangu wanajuana na hata wanakaribishwa kuwatembelea watoto wao kwa wakati mmoja na ikiwa umeoa, unakaribishwa kuja na mkeo.

Kinachonifanya kufaulu katika maisha haya ni kwa sababu mimi hushiriki katika uhusiano mmoja baada ya mwingine kuhakikisha kwamba sichanganyikiwi inapowadia wakati wa kumtambua baba halisi wa mtoto nikishika mimba.

Huenda sitakuwa na uwezo wa kutimiza ndoto yangu ya kuzaa na dume kutoka kila kaunti lakini niko tayari kuwakabidhi mabinti zangu jukumu la kuendeleza ndoto hii watakapokomaa”.