FUNGUKA: ‘Mahaba ya video yanitosha’

FUNGUKA: ‘Mahaba ya video yanitosha’

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA jamii nyingi, mahaba, kwa viwango vya kawaida, huhusisha mgusano baina ya wapendanao.

Lakini huku wengine wakifurahia mgusano huu, kwake Mikael mambo ni tofauti kabisa. Kwa Mikael, japo kihisia anaweza mpenda mwanamke tena kwa dhati, kwake, mgusano ni jambo ambalo katu halimo katika ulimwengu wake wa mapenzi.

Mikael ni mwanamume wa miaka 53. Yeye ni baba wa watoto wawili. Kifungua mimba wake ni binti wa miaka 21, ilhali mwanawe wa pili na mwisho ni mvulana wa miaka 17. Kwa sasa hana mke kwani walitalikiana miaka mitano iliyopita.

Mikael amesomea masuala ya teknolojia ya uhifadhi wa mitambo ya kielektroniki, ambapo kwa zaidi ya miongo miwili, amekuwa akifanya kazi na mashirika mbali mbali ya kimataifa.

Kazi yake imemwezesha kusafiri katika nchi mbali mbali barani na mbali. Na katika harakati hizo amejizolea pesa nyingi, na kuwekeza katika nyanja mbali mbali. Ana majumba ya kifahari na magari ya uchukuzi miji ya Mombasa na Nairobi.

Mbali na ufanisi wake, kuna jambo lingine kuhusu jamaa huyu ambalo huwaacha wengi wanaomfahamu vinywa wazi:

“Sifurahii mgusano wa aina yeyote wakati wa mahaba. Badala yake, kiu yangu ya mahaba inamalizwa kupitia video.

Nikisema haya namaanisha kwamba naam naweza mpenda mwanamke, lakini pindi baada ya uhusiano kung’oa nanga rasmi, suala la mgusano au hata kuonana ana kwa na halipo.

Badala yake, tunamalizia mambo yote kwa kuonana kupitia video. Lakini hii haimaanishi kwamba ule msisimko wa mahaba umekatizwa hapa.

La! tunadumisha mazingira ya mahaba kila inapohitajika. Ikiwa ni kuzungumziana kwa sauti za upole, kupapasana, kubusiana na hata hatimaye kushiriki mahaba, yote tunayafanya kupitia video.

Hii inamaanisha kwamba ukiwa mpenzi, mchumba au mke wangu, hatutaishi katika nyumba moja. Mimi katika nyumba yangu simruhusu mwanamke. Badala yake, niko tayari kukununulia nyumba yako, mbali na ninakoishi, ambapo kila jioni baada ya kazi, tutakuwa tukikutana na kumaliza shughuli zetu zote kupitia kwenye video.

Ili kufanikisha haya, chumba changu cha kulala kina kamera katika kila pembe, ambapo binti akikubali kuwa mchumba wangu, pia nitahakikisha kwamba chumba chake cha kulala kimewekwa mitambo hii.

Kwangu, mahaba ya video yanitosha na sina nia ya kubadilisha kauli yangu kuhusiana na mbinu hii yangu. Sina haja na watoto zaidi kwa hivyo ukiamua kuwa mpenzi au hata mke wangu, sahau suala la uzazi.

Kumbuka kwamba niliwahi kuwa na mke ambaye nilimuoa tu kwa minajili ya kunizalia. Pindi baada ya kunizalia wanangu wawili, huduma zake za kimwili ziliisha ambapo kilichosalia tu kilikuwa kushibisha uchu wangu kupitia video.

Mwanzoni, mke wangu alijaribu kukubaliana na mapendekezo yangu, lakini muda ulivyokuwa ukisonga, alishindwa kustahimili matakwa yangu, na hivyo kuamua kushika njia. Kwa hivyo hata wewe ukija, usitarajie mambo kuwa tofauti.”

You can share this post!

GSU na KPA nje ya vita vya medali, watawania sasa nafasi...

Mfumo wa haki wa kitamaduni waokoa kaka walioua jamaa