Makala

FUNGUKA: ‘Mbona niumie na nimebeba mgodi?’

October 12th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

UKIWA shuleni au chuoni kusoma kwa bidii ndiyo hakikisho la ufanisi na ajira siku za usoni.

Hata hivyo, kwa Masingu hiyo ni ndoto.

Binti huyu anaamini kwamba ikiwa wewe ni mwanamume, basi uwezo wako wa kupaa katika ngazi ya madaraka kazini itategemea na kiwango chako cha kuwa kibarakala wa wakubwa wako.

Na ikiwa wewe ni binti, kuwa kibarakala au ‘mkarimu eti’ wa kugawa asali kutakupa nafasi yoyote kazini.

Na kutokana na hayo, binti huyu amepiga nakshi weledi wake wa kuwarambisha asali wakubwa wake kazini; suala ambalo kwa miaka limemhifadhia wadhifa mkubwa kazini, na hivyo kumhakikishia mshahara mnene.

Masingu ameweza kudumisha wadhifa wake katika kampuni iliyomuajiri kwa takriban miongo miwili, huku akiendelea kupandishwa madaraka kila orodha ya wanaoongezwa taji inapotolewa mwanzoni wa mwaka.

Hii ni licha ya kwamba kisomo chake ni duni. Na sio kwamba ni wale watu maalum walio na werevu wa kuzaliwa. La, Masingu ni mpumbavu kiasi cha kwamba hata kazi haielewi vyema. Wakati mmoja alialikwa katika warsha ya kimataifa iliyohusisha wataalam katika nyanja inayomhusu ambapo ujinga wake ulijitandaza waziwazi na kuwaacha kinywa wazi washiriki huku akiaibisha mwajiri wake. Kwa hivyo siri ni nini?

“Siwezi tia bidii ilhali nina chombo cha kurahisisha kazi yangu. Hiyo ndio imekuwa kauli yangu tangu nilipojiunga na shirika hili kama msichana mdogo.

Kwa hivyo tokea zamani, nimekuwa nikitumia chombo hiki kama ngazi ya kunipandisha popote nataka kwenda.

Nilipoajiriwa nilianza kwa kuwatongoza wafanyakazi wenzangu ambapo kazi yao ilikuwa kuninunulia lanchi na kugharimia mahitaji yangu ya kifedha, huku mshahara wangu mdogo nikiutumia kwa kazi zingine. Aidha, walikuwa wakinifanyia kazi hasa ikizingatiwa kwamba sikuwa naelewa mambo.

Muda ulivyosonga, mahitaji yalibadilika na wafanyakazi wenza hawakunifaidi tena. Kwa hivyo nikaanza kuwatongoza wakuu wa idara, ambao walikuwa wakifunika udhaifu wangu na kuhakikisha kwamba japo sina ujuzi, jina langu halikuonekana kwenye orodha ya waliofaa kufutwa kazi kila kulipokuwa na mipango ya kupunguza wafanyakazi.

Nikiona kana kwamba mkuu wa idara kidogo anarusha jicho kwingineko au ananipuuza, basi nilikuwa namtafuta aliye juu yake na kumtongoza, na ni yeye alikuwa mtetezi wangu kazini.

Nilisomea diploma chuoni na kwa sababu nilijua kwamba sikuwa mwerevu, sikuona haja ya kuendelea na masomo hivyo nilianza kuwatongoza mabosi. Hakuna bosi hata mmoja ambaye hajapitia mikononi mwangu.

Huku wengine wakiwa na shahada za digrii, uzamili na hata uzamifu, au wakiwa na ujuzi wa kikazi, nimekuwa nikipanda madaraka na kuwaacha pale pale.

Sijaolewa wala sina mtoto kwani familia ingekuwa kizingiti kwangu. Kwa sasa miaka inazidi kuongezeka na umri wangu umesonga kwelikweli na sina matumaini ya kuafikia hayo.

Lakini sijuti kwani nimewekeza kifedha, nina nyumba, gari na biashara kadha wa kadha ambapo hata nikiachishwa kazi, sitakumbwa na changamoto za kifedha”.