Makala

FUNGUKA: Mimi ni kahaba mchana lakini mke wa mtu usiku

November 14th, 2020 2 min read

NA PAULINE ONGAJI

Kwa wengi, ukahaba mara nyingi hutokana na umaskini. Lakini sio kwake Bi Merita. Bibi huyu ameamua kufanya kazi hii licha ya kuwa ana taaluma ya kifahari na ameolewa na dume lililo na mfuko mzito na mama wa watoto wanne

Merita ni binti wa miaka 34 na amekuwa akifanya kazi hii kwa zaidi ya mwongo mmoja. Ni mkazi wa Pwani. Yeye ni msomi ambapo ana shahada ya uzamili katika masuala ya biashara na hata ana ajira nzuri tu.

Ni mkurugenzi msimamizi wa biashara katika shirika moja mjini Mombasa. Mumewe ni mfanyabiashara maarufu na anamiliki majumba na magari kadha wa kadha.

Kimapato, familia hii haina upungufu wa pesa na mumewe amekuwa akikidhi vilivyo mahitaji ya wanawe. Lakini hilo halijamzuia Merita kuendesha shughuli za ukahaba, kazi ambayo amekuwa akiifanya kwa usiri mkuu.

“Nimebobea katika masuala ya ukahaba ambapo wateja wangu wengi ni watalii wa kigeni.Mimi huwa nafahamiana na wateja wangu mitandaoni hata kabla ya wao kufunganya virago na kuzuru humu nchini.

Ni katika mazungumzo haya ambapo pia masuala ya malipo hushughulikiwa, kumaanisha kwamba baada ya shughuli kila mtu anaenda zake pasipo manung’uniko.Hii pia inasaidia kuzima shaka tunapokutana kwa mara ya kwanza.

Mara nyingi shughuli zetu huisha mchana, nyakati rasmi za kazi, ambapo ni vigumu sana kwa wanaonifahamu, na hasa mume wangu kufuatilia mienendo yangu.Kazi yangu nzuri imenifanya kusakwa sio tu na watalii wa kizungu, bali pia mabwenyenye kutoka humu nchini wanaozuru ufuoni wakiwa likizoni.

Wengi wao hunipigia simu kupanga jinsi watapokea huduma hizi pindi wanapofika mjini.Kuna wale wanaoniuliza kwa nini nafanya ukahaba ilhali pamoja na mume wangu tuna pesa? Ila mimi huwajibu kwa kuwauliza swali hili; je, ni wakati gani pesa zimewahi kutosha?

Pesa na zawadi

Kila wakati nikiishiwa na pesa, ninachohitaji ni kuwapigia wateja wangu simu tu, na muda si muda napokea senti katika akaunti yangu. Kumbuka kwamba katika haya yote, mume wangu pia ananishughulikia vilivyo kifedha kama mkewe.

Nimepokea pesa na zawadi za fedha na mali kutoka kwa wateja wangu, rasilimali ambazo mume wangu hafahamu kwamba namiliki.Kuna mmoja ambaye ameninulia jumba katika eneo la Lamu, mwingine ameninunulia gari la kifahari, na mwingine anaendelea kunijengea jumba la kukodesha katika mji fulani huku huku Pwani.

Mbali na pesa, kiu yangu inatokana ni ile raha tu ya kutumbuiza wageni. Mume wangu hajui nina ‘Side hustle’. Anachojua ni kwamba nikiondoka nyumbani huwa naelekea kazini nilikoajiriwa.

Kawaida mimi hurauka kwenda kazini alfajiri na mapema, hivyo hakuna anayeweza shuku nina shughuli ziada.Aidha huwa simpi mume wangu nafasi ya kunishuku kwani huhakikisha kwamba kila anapowasili nyumbani, anapata nishafika.

Nafanya majukumu yangu yote ikiwa ni pamoja na kumwandalia chakula, vilevile kumshibisha kimahaba”.