FUNGUKA: ‘Navutiwa na kijinyanya’

FUNGUKA: ‘Navutiwa na kijinyanya’

Na PAULINE ONGAJI

HUENDA waliosema kwamba penzi ni kikohozi walisema hivyo wakimuwazia Dominic.

Bwana huyu ana umri wa miaka 32 na ni muuguzi katika hospitali moja jijini Nairobi.

Licha ya kuwa mtanashati ajabu na kisomo cha wastani, kaka huu ameduwazwa na penzi la ajuza mmoja wa miaka 75. Ajuza huyu humtumia na kumsukuma kufanya mambo ambayo yamekuwa yakiwashangaza wengi wanaomfahamu Dominic.

Kwanza kabisa ajuza huyu alimshawishi kuchukua mkopo wa Sh1M kutoka benki ili kufadhili masomo ya mjukuu wake ambaye anasomea shahada ya uzamili katika chuo kikuu kimoja jijini Nairobi.

Aidha, mbali na kuwa kaka huyu ndiye anayeshughulikia gharama zote za nyumbani wanakoishi katika mtaa mmoja jijini Nairobi, yeye pia ndiye anamsomeshea wajukuuze wanne.

Pia, ajuza huyu amekuwa akimtumia Dominic kama chambo kunasa mabinti wenye mifuko mizito ili naye pia anufaike kutokana na pesa wanazompa kama anavyosimulia kaka huyu.

“Kila Ijumaa lazima tutembelee baadhi ya klabu za kifahari katika upande mwingine wa jiji la Nairobi ambapo bibi huyu hujifanya kuwa nyanyangu, na kutokana na sababu kuwa mimi ni kivutio cha wanawake

wengi, basi tunatumia uzuri huu kunywa bia za madume wengine.

Aidha, mara kwa mara amenishawishi nitumie uzuri wangu ili kunasa mabosi wa kike ili nao waweze kuwasakia wajukuuze kazi. Mwaka jana baada ya wajukuuze wawili kukamilisha chuo kikuu, walikuwa na changamoto ya kupata ajira.

Kama Wakenya wengi wasio na mwunganisho, walikabiliwa na ugumu wa kukutana na bosi fulani wa kike katika kampuni aliyokuwa anataka waajiriwe.

Ili kumshawishi bosi akutane nao, alinituma kumtongoza bosi huyo ambaye bila shaka alichanganyikiwa na uzuri wangu pindi aliponiona. Baada ya kufanikiwa kuwakutanisha naye, nami nilihitajika kumtumbuiza kama malipo. Baada ya kumburudisha mara kadhaa, mabwana hao waliajiriwa.

Pengine unajiuliza nini hasa kinachonifanya kumtii bibi huyu anayetosha kuwa nyanyangu? Kwanza, sio suala la kiumri. Nampenda sana ajuza wangu huyu.

Anachonipa, hawa mabinti barubaru hawawezi fikia. Burudani yuanipa bila kipimo, kwa mtindo wowote ule niupendao, wakati wowote, bila kulalamika. Kumbuka na hii ni baada ya kunikanda kwa maji moto usiku kucha.

Isitoshe, chakula changu ni yeye hunipikia, tena kwa mbinu ya kipekee na kuandaliwa kwa ustadi mkubwa.

Nguo zangu zinafuliwa kwa uangalifu huku zikipuliziwa marashi wakati wa kupaswa.

Ninaporejea nyumbani usiku wa manane kutoka kazini, huwa ameningoja kwenye kituo cha magari ili kunilinda kutokana na wezi, ishara kuwa ananipenda sana.

Kwa ufupi, penzi lake japo la ajuza, halina kipimo, na ninachofanya ni kulipiza wema kwa wema”.

You can share this post!

CHOCHEO: Ukikutana na EX itakuwaje?

MWANAMUME KAMILI: Karibu kijiweni tuwakemee wanaotafuta...