Makala

FUNGUKA: 'Nimeingiza wanne boksi'

February 23rd, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

KWA jamii nyingi ndoa ni baina ya mwanamume na mke mmoja. Hata kwa zile zinazoruhusu waume kuwa na wake zaidi ya mmoja, mara nyingi huwa sio siri huku wanawake wahusika wakijuana n ahata kutambulika na jamaa za dume lililowaoa.

Hata hivyo, kwa Gareth, hizo ni hekaya za Abunuwasi.

Bwana huyu, mfanyabiashara mjini Nakuru, ameoa wanawake wanna kutoka kaunti tofauti nchini, na ajabu ni kwamba kila mmoja anadhani yeye ndiye mke wa kipekee wa dume hili.

Kwanza kabisa Gareth anamiliki biashara ya magari ya usafiri wa abiria na malori ya kusafirisha mizigo, suala ambalo huenda limemwezesha kuendeleza ulaghai wa kimapenzi kwa ujanja ambapo kwa zaidi ya miaka kumi amekuwa mume wa wake wanne wasiojuana.

Nina wake wanne, Alice, anayeishi mjini Nakuru, Kate mwenye makazi jijini Nairobi, Irene aliyekita kambi mjini Eldoret na Evelyn anayeishi mjini Kakamega, wanawake kati ya umri wa miaka 39 na 47.

Pamoja tumejaliwa watoto wanane huku kila mke akiwa amenizalia wana wawili.

Biashara yangu imeniwezesha kushughulikia kila mmoja ambapo wote nimewajengea majumba ya kifahari, kuwanunulia magari na ni mimi mwenyewe ndiye ninayeshughulikia mahitaji yao ya kila siku.

Hata hivyo wote wana taaluma au biashara zinazofanya vyema sana kumaanisha kwamba sio pesa zangu zilizowavuta kwangu.

Alice ni mwalimu wa shule ya sekondari, Kate ni mhadhiri katika chuo kikuu kimoja nchini, Irene anamiliki biashara kubwa ya kuuza vifaa vya kielekroniki, simu na vipuri vyake, ilhali Evelyn ni mkuu wa wahudumu wa kiafya katika hospitali moja nchini.

Hakuna mmoja kati yao anayejua mwingine, au hata kushuku kwamba nina wake wengine nje, suala ambalo limewafanya marafiki zangu kuniandama na maswali kila mara; je nafanikiwa vipi?

Nidhamu

Mojawapo ya sababu ambazo zimenifanya kufanikiwa katika mchezo huu wangu ni nidhamu kuu.

Nina simu tano; moja ni ya kibiashara ambayo hakuna kati ya wake zangu anayoifahamu. Kisha hizi nne ni binafsi ambapo kila mke anafahamu nambari moja kati yazo.

Nikiwa jijini Nairobi natumia simu ambayo Kate pekee anaifahamu, nikiwa Nakuru natumia nambari ambayo Alice pekee anaifahamu, nikiwa Eldoret natumia nambari ambayo Irene pekee anaifahamu huku nikiwa Kakamega natumia nambari ambayo ni Evelyn pekee anaifahamu.

Mbali na hayo nimejifunza kuwapa heshima wake zangu kiasi cha kufanya iwe ngumu kwa yeyote kushuku kwamba wako kadha. Sitembei na simu hizo zote ambapo kila ninapomwendea mke mmoja nabeba simu ya nambari anayojua, na ile ya kibiashara huku hizo zingine nikiziacha na kuzizima.

Pia, nimewafunza kwamba biashara yangu hainiruhusu kushika simu wakati mwingine, na ni mimi pekee ninayeweza wapigia siku au kuwaashiria wakati wa kunipigia simu.

Aidha, nimebobea inapowadia wakati wa kubadilika kila nikiwa na mke mmoja. Ni suala ambalo limeniwezesha kutochanganyikiwa na kumuita mwingine kwa jina la mwenzake.

Pia, kipawa hiki kimeniwezesha kukidhi mahitaji ya kimahaba kila mke, na hivyo kuzima mawazo ya kuwa huenda mimi hushiriki mechi za mbali.