Makala

FUNGUKA: 'Nimezoea vya kunyonga…’

November 28th, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA ulimwengu wa sasa ambapo visa vya wanaume kukwepa majukumu ya malezi vimekuwa vya kawaida, ni nadra kumpata kaka aliyejitolea kujitwika jukumu la kuwalea watoto wa dume lingine.

Lakini kwa Jose, mambo ni tofauti sana. Kwanza kabisa acha nikupe maelezo kuhusu kaka huyu. Jose ni mwanamume wa miaka 49. Yeye ni afisa wa masuala ya kibiashara katika shirika moja la kimataifa jijini Nairobi.

Kazi hii ambayo ameifanya kwa zaidi ya mwongo mmoja, imemwezesha kufanikiwa kimaisha kutokana na mshahara mkubwa ambao amekuwa akipokea.

Aidha, kimaumbile, Mungu kamjalia. Amenadhifika kutoka utosini hadi nyayoni. Kutokana na uzuri wake vile vile rasilimali alizo nazo, wengi wanamtarajia kuchagua mabinti wa viwango vya juu sio tu kimaumbile, bali pia kielimu na kitaaluma.

Lakini Jose kafanya kufuru; chaguo lake ni kinyume kabisa na matarajio na dhana ya jamii.

“Napenda wanawake wenye viwango vya chini zaidi kimasomo, kimwonekano na zaidi ya yote, lazima binti awe na watoto. Na ninaposema watoto simaanishi tu mtoto mmoja au wawili. Ninapomsaka binti, sharti awe na angaa watoto watatu. Mbali na hayo, lazima watoto hawa wawe na baba tofauti. Hili ni muhimu kwani inapunguza uwezekano wa dume kujitokeza na kudai kwamba binti huyu ni mkewe.

Jasiri

Suala la mwonekano na kisomo ni mada ya siku nyingine. Lakini leo acha nizungumzie kwa nini navutiwa sana na wanawake ambao tayari washazaa watoto kadhaa.

Kwanza kabisa hawa ni wanawake waliowajibika kwani uzoefu wao wa malezi umewafanya kuwa thabiti kimawazo wanapofanya maamuzi.

Aidha, mwanamke wa aina hii hana muda wa kukufanyia mzaha katika uhusiano.

Lakini cha muhimu ni kwamba wana uzoefu katika masuala ya mahaba. Huyu ni mwanamke ambaye ameonja uhondo chumbani angaa mara tatu, kumaanisha kwamba ana weledi si haba katika masuala ya mahaba.

Mnapoingia naye chumbani, anajua cha kufanya sio tu kukuridhisha, bali pia yeye mwenyewe kujipa raha wakati huu.

Kando na masuala ya mahaba, ni rahisi kunasa penzi la binti wa aina hii hasa ukifanikiwa kuwa na uhusiano wa karibu na watoto wake.

Hii inamaanisha kwamba hata anapotaka kuachana nawe, atatafakari kwa kina kabla ya kufanya hivyo kwani hataki kuvunja mwunganisho uliopo kati yako na watoto wake.

Pia mwanamke aliye na mtoto ni hakikisho kwamba ana uwezo wa kushika mimba, endapo utamhitaji akuzalie.

Aidha, nawaona kuwa majasiri kwani hawa ni wanawake ambao baada ya kushika mimba, hawakusita kutupilia mbali ujana wao na kuamua kuzaa, tofauti na wengine wanaojidai kuwa mabinti wachanga, ilhali wameavya mimba kadha wa kadha.

Kwa mfano, mwanamke ninaye mchumbia kwa sasa ni mama wa watoto sita. Nilikutana naye mwaka jana tayari akiwa na watoto hawa, tukapendana na sasa tunapanga kuoana mwaka ujao.

Ushauri wangu kwa vijana barubaru ambao hawajapata jiko ni kuwa, ukitaka amani, hawa ndio wanawake unaopaswa kuwalenga”.