Makala

FUNGUKA: ‘Ninavyonyaka mabosi wa kike kazini'

September 12th, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

TANGU jadi, mabinti ndio wamekuwa wakitarajiwa na jamii kutumia maumbile yao kujinufaisha.

Lakini sio kwa ulimwengu wake Festus. Kabla ya kusema lolote hebu kwanza nikutambulishe kwa kaka huyu. Festus ni mwanamume mwenye umri wa miaka 33, mkurugenzi wa masuala ya biashara katika shirika moja hapa nchini.

Yeye ni kaka mtanashati na hivyo amekuwa kivutio cha mabinti wengi anaokutana nao kila aendako.

Ameumbwa akaumbika kwani mbali na sura yake ya kupendeza, ana mwili wa kuvutia, sifa ambayo imezidishwa na bidii yake ya kufanya mazoezi kila mara.

Nasikia fununu kwamba kimahaba si mchache kwani ni wachache mno anaovuka nao chumbani humsahau.

Aidha kiakili amepiga msasa ufahamu wake wa masuala hasa kuhusiana na taaluma yake.

Kazini, yeye ni kivutio cha mabosi wake wa kike, na hata kuna uvumi kwamba hii ndiyo sababu kuu ambayo imemfanya kukwea ngazi kwa kasi kama anavyokiri.

“Kila wakati bosi wa kike anapojiunga na kampuni yetu, huwa niko tayari kutumia sifa hizi zote kumnasa katika penzi langu ili angalau hata mie nifaidike. Kinachonisaidia ni kwamba tangu jadi shirika letu limekuwa likizingatia uajiri wa wasimamizi wa kike.

Pengine unashangaa ninawezaje kumuingiza bosi boksi na bado niendelee kufanya kazi naye? Ni rahisi sana. Tunapoletewa bosi mpya, nahakikisha kwamba uwepo wangu unahisiwa. Ni lazima nitembee karibu na afisi yake kila wakati. Si wajua tena kimaumbile mimi si mchache, hivyo lazima atanitupia jicho.

Aidha, wakati wake wa kuingia afisini, mimi huhakikisha kwamba tunakutana. Niko tayari kugharimika kwa kulipia maegesho ya magari katika nafasi iliyotengewa wakubwa. Hii ni muhimu kwani itanisaidia kumfikia bosi kwa urahisi anapoingia kazini.

Pengine unajiuliza nitafanikisha hilo vipi? Ninapowasili mapema, mimi huketi ndani ya gari langu na kumsubiri na pindi anapofika, hushuka na kumuamkua huku nikitabasamu kisha kuandamana naye hadi afisini.

Na mkutanoni pia, siachwi nyuma kwani huhakikisha nachangia hoja zote hadi anitambue.

Nikishamnasa, basi napata fursa ya kuzungumza naye kila wakati na kufanikiwa kumshawishi kwamba mimi ni rafiki wala si adui yake kazini japo ni mgeni. Muda si muda mazungumzo huwa mepesi na hapa ninapata fursa ya kumuomba nimpeleke deti. Baada ya deti ya kwanza na ya pili, ndipo uzuri wangu katika nyanja zote utajitokeza na hivyo kuniwezesha kujishindia penzi lake.

Na kila ninapompagawisha, ndivyo najijengea nafasi bora ya kupandishwa madaraka, kuongezewa mshahara na kuimarishiwa masharti ya ajira hadi atakaponichosha kisha nitamtema kama ganda la mua.

Ni mbinu ambayo nimekuwa nikitumia tangu niajiriwe ambapo katika kipindi cha miaka saba, imeniwezesha kukwea hadi kwenye wadhifa wa usimamizi na hata kuwaacha nyuma walionitangulia kazini.

Ni shughuli ambayo nimeifanya tokea chuoni ambapo mabinti walipokuwa wakitumia uzuri wao kujizolea alama za masomo, hata mimi sikuachwa nyuma.

Kwa upande wangu, nakumbwa na jukumu la kuhifadhi usiri. Kwa mfano, sikubali jumbe kupitia simu au mitandao ya kijamii kwani ni rahisi kwa taarifa za mawasiliano yetu kudukuliwa. Mawasiliano yetu ni ya ana kwa ana na mara nyingi namhakikishia mwenzangu kuhusu usiri wa uhusiano wetu, ahadi ambayo sijawahi kuvunja.

Kwa wale ambao huenda wananihukumu, swali langu ni hili; Mabinti hutumia uzuri wao kujitafutia makuu, mbona sisi madume tusifanye hivyo?”