Makala

FUNGUKA: Ole wenu mnaoingia mtegoni…

April 4th, 2018 2 min read

Narekodi kila tukio, nahifadhi kila arafa kwa minajili ya kuwapaka tope endapo watajifanya wajanja kiasi cha kuasi ahadi walizotoa waliporusha ndoano. Wamezoea kuramba na kutema ving’asti hata kabla ya kutekeleza maafikiano yao
-Machere

Na PAULINE ONGAJI

Anapotembea ni vigumu kutomtambua kutokana na mienendo yake ya madaha na kelele anazosababisha sakafuni kwa kukanyaga kwa mshindo kwa viatu vyake vya visigino virefu.

Naam huyo ni Machere, binti ambaye amejiundia sifa kutokana na tabia zake za kuvizia madume huku umbo lake la kupendeza likiwazuzua mabwenyenye kwa walala hoi anakofanya kazi.

Lakini ole wao walala hoi kwani binti huyu kamwe hana haja na kaka asiye na mapeni. Kipusa huyu anavutiwa na mabwenyenye katika kampuni anamofanya kazi; yaani mameneja ambao mshahara wao unatikisa akaunti ya benki kila mwisho wa mwezi.

Amenasa kadha ambapo kila mmoja anayeingia kapuni mwake amepewa jukumu la kifedha analopaswa kuwajibikia. Kuna anayemlipia nyumba, kuna aliyemnunulia gari na kunaye anayemlipia karo chuoni ambapo anasomea shahada ya uzamili.

Nao wamehakikishiwa uhondo kutoka kwake kwani anatambulika kwa weledi wake wa kupakua bila choyo. Lakini kuna tatizo moja hapa, unaponaswa na penzi la Machere unapaswa kuwa mwangalifu kwani amejaa hila.

Binti huyu amebobea katika masuala ya kunakili na kurekodi kila kitu kinachoendelea katika uhusiano wake huku akihifadhi video za mahaba, jumbe za arafa na picha anazopigwa na hawa madume. Pengine ungependa kujua kwa nini hasa yeye hufanya hivi?

“Mimi ni mjanja! Usidhani nilifika nilipo kwa upumbavu. Nina nyumba, kazi ya mshahara mnono na gari, mali ambayo imetokana na werevu huu.

Narekodi kila tukio, nahifadhi kila arafa kwa minajili ya kuwapaka tope madume hawa endapo watajifanya wajanja kiasi cha kuasi ahadi walizotoa waliporusha ndoano.

Wamezoea kuramba na kutema hata kabla ya kutekeleza maafikiano yao. Kwa mfano kuna dume lilikuwa linataka kuhepa mkataba tuliowekeana ambapo nilipaswa kumrambisha uhondo huku naye akikumbwa na jukumu la kuhakikisha kuwa napandishwa madaraka kazini.

 

Dume kuhepa

Lakini baada ya kurambishwa asali dume lilihepa na hata kuhakikisha kuwa napoteza ajira. Ole wake kwani halikujua kuwa nilikuwa nimehifadhi arafa ambazo lilikuwa likinitumia, vilevile video na picha tulizopigwa tukiwa pamoja.

Siku ambayo nilishuku kuwa nilikuwa napaswa kupewa barua ya kuniachisha kazi, nilielekea afisini mwake na kumwonyesha huku nikitishia kuziwasilisha kwa mkewe.

Siku hyo hiyo niliitwa katika afisi inayohusika na kuajiri wafanyakazi na kuambiwa kuwa uamuzi wa kuniachisha kazi ulikuwa umebatilishwa.

Ili kufanikisha njama zangu, nimewekeza katika programu ya kisasa iliyo na uwezo wa kurekodi mjadala kwenye simu. Pia kila ninapoingia katika uhusiano lazima nihakikishe kuwa nahifadhi kila ujumbe na picha.

Tukiingia katika uhusiano, nahakikisha kuwa matukio yetu ya mahaba yanafanyika nyumbani ili niweze kunasa matukio kisiri. Hapa nimeweka kamera katika kila chumba na hasa cha kulala, kumaanisha kuwa narekodi kila kinachoendelea humo.

Kamera hizi ni za kurekodi shughuli za aina yoyote na nazihifadhi kama ushahidi endapo dume litajaribu kuepuka bila kutimiza ahadi zake.

Najua kunao wanaonihukumu lakini ningependa kuwafahamisha kuwa ujanja huu umenihakikishia ajira ya pesa nzuri japo mara nyingi sifanyi kazi.

Kadhalika werevu huu umenipa nyumba, gari na kuniimarisha kimasomo kila kuchao. Nani asiyetaka maisha ya raha na starehe?”