Makala

FUNGUKA: 'Rangi nyekundu hunisisimua ajabu…'

June 1st, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

KAMA wasemavyo, sawa na kikohozi, ni vigumu sana kuzuia mawimbi ya mahaba yanapovuma upande wako.

Aidha, watu huwa na mbinu mbalimbali za kunogesha na kudumisha mahaba.

Tumesikia kuhusu watu ambao mahaba yao yanachochewa na sura, kunao wanazuzuliwa na umbo, au hata werevu.

Lakini kwa Ben mvuto wake wa mahaba, kuambatana na viwango vya watu wengi, sio wa kawaida.

Kwanza acha nikupe maelezo mafupi kumhusu kaka huyu.

Ben ni mwanamume mwenye umri wa miaka 42, mkazi wa jiji la Nairobi.

Kwa miaka saba sasa amekuwa akihudumu kama msimamizi wa masuala ya kifedha katika shirika moja jijini humu.

Taaluma yake imemwezesha kujichumia mapato mazuri ambapo amewekeza katika sekta mbalimbali za kibiashara.

Kimaumbile, Ben ana kila sababu ya kumshukuru Mungu. Ni mtanashati tena mwenye umbo la kumezewa mate na mabinti, wengi wakitamani kuchumbiwa naye.

Lakini kwa wale wanaopata fursa ya kuingia kwenye mtego wake, kibarua huwa kukubaliana na mvuto wake usio wa kawaida wa kimahaba.

Ben ana tamaa za ajabu kimahaba. Yeye havutiwi na urembo wala umbo la binti, la hasha! Rangi, tena nyekundu humpa mnato wa ajabu.

“Rangi nyekundu ndo kichocheo changu cha mahaba, bila hiyo, hakuna jinsi ninavyoweza kujihusisha katika shughuli hii. Ndiposa vyumba vyote katika nyumba yangu vimepakwa rangi nyekundu ili endapo nitapata mgeni, basi nisibabaike.

Aidha, fanicha zangu kuanzia kwa viti, kabati, vyombo vya kieletroniki, malazi vilevile vifuasi kama pazia, mikeka, zulia na mapambo mengine ya nyumbani yote ni mekundu. Isitoshe, hata vyombo vyangu vyote ni vyekundu.

Pia, balbu nyumbani kwangu hutoa mwangaza mwekundu, bila kusahau mavazi yangu ambapo kuanzia kwa boksa, shati, longi, tai, viatu na hata saa ni nyekundu.

Nafanya hivi kwa sababu msisimko wangu kimahaba huchochewa na rangi hii na pindi ninapokumbana na rangi nyingine, basi hisia huzimika pap!

Penzi langu kwa rangi hii limeenda hatua zaidi kiasi kuwa kila ninapotembea njiani na nikutane na kidosho aliyevalia mavazi mekundu, basi macho hukwama pale na lazima nimwandame hadi anipe namba yake.

Lakini cha kushangaza ni kuwa tunapokutana wakati mwingine akiwa amevalia mavazi ya rangi nyingine basi, hamu hutoweka ghafla.

Rangi nyekundu balaa

Mvuto wangu unajulikana hata kazini kiasi kuwa warembo hapa hawaruhusiwi kuvalia mavazi ya rangi nyekundu kiholela, la sivyo nitawaandama kama siafu kwenye msafara wao.

Ndiposa ukitaka kuwa mpenzi wangu, sharti uwe tayari kuvalia nguo za rangi nyekundu kila siku kuanzia kwa chupi, sidiria, nguo, begi, viatu na hata saa, iwapo unataka kudumisha uhusiano huo, la sivyo shika hamsini zako.

Unapokubali kuwa nami na huna mavazi ya rangi hii, basi jambo la kwanza ni kwenda ‘shopping’.

Aidha kila siku lazima ujipake mapambo, kuanzia kwa lipstiki, rangi ya kucha, wanja na vipodozi vinginevyo vya rangi nyekundu”.