Makala

FUNGUKA: ‘Tabia zake chwara zanisisimua ajabu’

February 18th, 2019 2 min read

NA PAULINE ONGAJI

“Uzuri wa mwanamke sio urembo ni tabia,” maneno yake mwanamuziki Samba Mapangala, na kauli ambayo nina uhakika kwamba inaungwa mkono na madume wengi.

Lakini sio taswira ambayo William, kaka mwenye umri wa miaka 36 anayokubaliana nayo. Kwa mwanamaume huyu, mhadhiri katika chuo kimoja kidogo jijini Nairobi, hakuna kitu kinachosinya kama mwanamke mzuri.

Kulingana naye, mara nyingi hao wanaojidai kuwa wazuri hujifanya kuwa wema ilhali ndani wana uozo usioelezeka. Ni sababu hii inayomfanya kuwa mwangalifu anapomchagua binti wa kumchumbia ambapo kwake, lazima awe muovu ajabu.

“Nataka binti ambaye tabia zake ni chafu kiasi cha kutokubaliwa na jamii. Namtaka kipusa ambaye nikimnunulia chupa nzima ya mvinyo ataibugia pasi woga. Yaani binti aliye na mazoea ya kulewa chakari.

Kabla ya kumchumbia nitamtembeza katika klabu zote jijini kuona iwapo anafahamika na walinzi na wahudumu, kwani hiyo itaashiria kwamba yeye ni mteja pale na hivyo atakuwa amepita mtihani wa kwanza.

Pili, katika masuala ya mahaba, namtaka binti asiye na haya kutumbuiza. Simtaki binti bikira. Namtaka kipusa aliyewatumbuiza madume wengi kwani hilo ni hakikisho la uzoefu wake katika masuala ya mahaba.

Sitaki kusumbuana na binti nikimfunza mitindo tofauti wakati wa mahaba. Kipusa anayegawa asali pasi uchoyo au aibu ya kuwa huenda jina lake likachafuliwa ndo raha yangu.

Binti ambaye ana historia ya kumegwa na madume kadha wa kadha. Sifa hii inamfanya kubobea katika masuala ya kimapenzi kwani amekuwa katika uwanja huo bila soni.

Namtaka binti aliyeonjwa kwingi, kumaanisha kwamba ana ufahamu wa ladha tofauti, na hivyo pindi nitakapoamua kumuoa, hatakuwa na uchu wa kutaka kufahamu madume zaidi.

Sifurahishwi na mabinti wanyamavu. Napenda msichana anayepiga kelele klabuni sio tu kwa mazungumzo bali pia kwa vicheko, suala linalofanya uwepo wake kutambuliwa. Binti ambaye anajua kurusha matusi, mwanamke ambaye nikitembea naye hakuna anayeweza kunichokoza kwani amenoa ulimi tayari kushambulia.

Binti aliyepaka nywele zake za sehemu zote mwilini rangi zisizo za kawaida kama vile manjano. Kipusa aliyejitoboa sehemu zote za masikio na maeneo mengine mwilini ikiwa ni pamoja na mdomo, ulimi na kitovu.

Binti asiyejihusisha na masuala ya kidini kamwe.

Je, ni nini kinachonivutia kwa vipusa wa aina hii? Mabinti wa sampuli hii ni wakweli, halisi na kama wasemavyo, ‘what you see is what you get’.

Ukiwa katika uhusiano naye hauna wasiwasi kwamba wakati mmoja mambo yatakuwa mabaya kwani yeye mwenyewe ni mbaya ajabu”.