HabariSiasa

Funzo kwa Uhuru

February 21st, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta angekuwa kama mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, basi hangekuwa akilalamika kuhusu mawaziri na maafisa wanaozembea kazini ama kumuaibisha machoni pa wananchi.

Majuzi Rais Kenyatta alitangaza atakuwa akifuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo mwenyewe akilalamika kuwa aliopatia kazi wamemvunja moyo.

Tofauti na Kenya ambapo mawaziri wana mazoea ya kutoa habari za kukanganya ama kupotosha, nchini Rwanda mawaziri kuegesha magari maeneo yasiyoruhusiwa ama kukataa kukaguliwa wanapoingia katika majengo na maeneo ya umma ni sababu tosha ya kuwafanya wafutwe kazi.

Hii ilikuwa sababu tosha kwa Rais Kagame kumfuta kazi waziri wa haki Evode Uwizeyimana kwa kukataa kukaguliwa alipokuwa akiingia jengo la umma na kuwa na mazoea ya kuegesha gari eneo lisiloruhusiwa.

“Evode aliegesha gari lake eneo ambalo watu hawafai kuegesha, kisha akajaribu kuingia katika jengo bila kukaguliwa. Mlinzi alimfuata na kumwambia kwa upole kwamba alipasa kukaguliwa lakini akampiga na kumwangusha chini,” alisema Rais Kagame.

Hapa Kenya mawaziri na maafisa wakuu serikalini wamekuwa watovu wa nidhamu na wavujaji sheria bila kupepesa macho.

Hii imekuwa ikizua malalamiko hasa barabarani ambapo magari yao huendeshwa mkondo wa barabara usioruhusiwa huku walinzi wao wakihangaisha watumizi wengine wa barabara kwa kuwatisha kwa bastola na kuwagongea vioo vya magari.

Pia hawafuati kanuni za kiusalama kama vile kukaguliwa wanapoingia kwenye majumba.

Badala ya mawaziri hao kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu, wanaojaribu kuhakikisha sheria inafuatwa ndio wanajipata motoni kama ilivyomtokea Bi Daizy Cherogony, ambaye alifutwa kazi kwa kumuomba Waziri Fred Matiangi kupanga foleni akaguliwe katika uwanja wa ndege wa JKIA.

Rais Kagame alisema waziri aliyefutwa kazi alikuwa ameonyesha tabia mbaya mara kadhaa. Hii ni tofauti na Kenya ambapo mahakama ilisema Bi Cherogoiny ndiye aliyekuwa na makosa.

Mwezi uliopita Saidi Musa Jobba alishtakiwa kwa makosa ya kusingiziwa baada ya kukataa kuondokea gari la mkuu serikalini lililokuwa likiendeshwa upande usiofaa wa barabara ya Langata jijini Nairobi.

Mapema wiki hii katika barabara hiyo ya Langata, mwendesha gari aligonga mtu aliyekuwa akitembea kando alipokuwa akihepa kugongana na gari la VIP lililokuwa likiendesha upande kinyume wa barabara.

Katika kuhakikisha mawaziri wake wanawajibika, Rais Kagame juzi alimfuta kazi waziri wa afya Diane Gashumba kwa kumdaganya kuhusu maandalizi ya nchi hiyo katika kukabiliana na Coronavirus.

“Alimwambia waziri mkuu kwamba tuna vifaa 3500 nchini. Baadaye tuligundua tulikuwa na vifaa 95 pekee. Nilipomuuliza alianza kunipa stori ndefu,” Rais Kagame akasema.

Ingekuwa Rwanda, Waziri wa Uchukuzi James Macharia hangekuwa kazini hasa kwa kutoa habari za kukanganya kuhusu mabasi ya mwendo kasi jijini Nairobi.

Naye waziri wa Utalii Najib Balala angekuwa amefutwa kazi kwa kutoa habari za kupotosha kuhusu vifo vya vifaru waliohamishwa kutoka mbuga ya Masai Mara hadi Tsavo mnamo 2018.

Bw Balala aliidhinisha kuhamishwa kwa vifaru hao licha ya wataalamu kushauri kuwa mazingira katika eneo hilo yalikuwa hatari kwa wanyama hao. Badala ya kuchukuliwa hatua aliwaambia wanaharakati wa wanyamapori “waende kuzimu.”

Tofauti na Kenya ambapo mawaziri wanaotajwa katika kashfa za ufisadi huendelea kuwa ofisini, Rais Kagame huwa anawafuta kazi mara moja.

Alimfuta kazi waziri wa Elimu Isaac Munyakazi kwa kukubali hongo ya Sh55,000 ili kubadilisha matokeo ya mitihani.