Michezo

Furaha iliyoje Faith Kipyegon akirejeshewa medali yake


Paris, Ufaransa

SAA chache tu baada ya kupokonywa usindi wa nishani ya Fedha katika mbio za mita 5,000, Bingwa wa Dunia, Faith Kipyegon Jumatatu, Agosti 5, 2024 alipewa medali hiyo baada ya maafisa wa timu ya Kenya kushinda kesi dhidi ya madai kwamba Kipyegon alimsukuma Gudaf Tsegay wa Ethiopia ikibakia mizunguko miwili.

Mshindi, Beatrice Chebet katika mbio hizo alimaliza kwa muda wa dakika 14:28.56, mbele ya Kipgyegon aliyetumia muda wa dakika 14:29.60, huku Sifan Hassan wa Uholanzi akimaliza katika nafasi ya tatu kwa dakika 14:30.61.

Dhahabu ya Chebet ilikuwa ya pili ya Olimpiki kwa Kenya tangu Vivian Cheruiyot aibuke bingwa mnamo 2016 Michezo hiyo ilipofanyika Rio De Janeiro.

Muda mfupi baadaye, Mary Moraa alijinyakulia nishani ya Shaba katika mbio za mita 800 akitumia muda wa dakika 1:57.42.

Mshindi wa mbio hizo alikuwa Keely Hodgkinson wa Uingereza aliyemaliza kwa dakika 1:56.72, wakati Tsiye Duguma wa Ethiopia akishinda medali ya Fedha.

Matokeo haya yanadhihirisha kuwa Kenya haijashinda nishani ya dhahabu katika mbio hizo tangu Pamela Jelimo aibuke mshindi mnamo 2008.