Habari MsetoSiasa

Furaha kwa Babu Owino hakimu kuamua hana kesi ya kujibu

September 11th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MBUNGE wa Embakasi Mashariki Paul Ongili ‘Babu Owino’ Jumatatu aliondoka mahakama ya Kibera, Nairobi akiwa na furaha baada ya kesi aliyodaiwa kumshambulia mpinzani wake kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 kuondolewa.

Mlalamishi, Joshua Otieno Obiende alifika kortini na kujulisha mahakama kwamba alitaka kuondoa kesi kwa sababu amemsamehe Bw Owino.

“Niko hapa kufahamisha mahakama kwamba ninataka kuondoa kesi. Nimemsamehe ndugu yangu Babu Owino. Yaliyotendeka sasa ni historia,” Bw Obiende aliambia mahakama.

“Sikulazimishwa na yeyote kuondoa kesi hii. Nimeamua kwa hiari yangu kwa moyo kwa undugu. Bw Owino anatoka Nyalenda na mimi ninatoka Ahero. Sisi ni ndugu. Mungu aliniagiza nimsamehe na kama Mungu anasamehe mimi ni nani kutomsamehe ndugu yangu,” Bw Obiende aliambia Hakimu Mkuu Joyce Gandani.

Alipoulizwa iwapo alilipwa chochote ili kuondoa kesi, mwanasiasa huyo aliyegombea kiti cha ubunge kwa tiketi ya chama cha Amani National Congress na kushindwa na Bw Owino, alisema ni Mungu atakayemlipa. “Sikulipwa chochote lakini Mungu atanilipa,” alisema.

Kabla ya Obiende kuingia kizimbani kuwasilisha ombi lake, wakili wa Bw Owino alijulisha mahakama kwamba pande zote zilikuwa zimesuluhisha tofauti zao. “Niko na furaha kuripoti kuwa pande zote zimekubaliana na mlalamishi anataka kuondoa kesi,” alisema wakili.

Babu alimshukuru Obiende kwa kumsamehe na kusema moyo wa undugu utaendelea. “Asante ndugu yangu kwa hatua hii,” alisema.

Pande zote mbili ziliwasilisha hati ya kiapo kortini kuthibitisha kuwa zilikubaliana kuondoa kesi. Obiende alikuwa amemlaumu Babu Owino kwa kumpiga na kumsababishia jeraha la kudumu katika kituo cha kupigia kura cha Soweto mnamo Agosti 8 mwaka jana. Babu alikanusha shtaka hilo. Katika shtaka la pili, ilidaiwa kwamba alimzuia Bw Obiende kupiga kura katika kituo hicho kinyume na sheria za uchaguzi.

Jana, upande wa mashtaka haukupinga ombi la Obiende lakini ukamkumbusha kuwa hataweza kurudisha kesi kortini siku zijazo. Hakimu Mkuu Joyce Gandani alikubali ombi hilo na kuagiza Bw Owino kurudishiwa dhamana yake ya Sh100,000. Baada ya kesi kuondolewa, Owino na Obiende walitoka nje ya korti na kuzungumza kwa muda kabla ya kuondoka.