Habari za Kaunti

Furaha serikali kupitia KPA ikianza kuwafidia wavuvi wa Lapsset mamilioni

June 4th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

IMEKUWA ni shangwe na vigelegele kwa wavuvi waathiriwa wa Mradi wa Bandari ya Lamu (Lapsset) baada ya serikali kupitia kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (KPA) kuanza kuwafidia maelfu ya fedha juma hili.

Kati ya wavuvi 4,125 wanaofaa kufidiwa, zaidi ya 1,000 tayari walikuwa wamepokea hela kwenye akaunti zao za benki kufikia Jumanne wiki hii.

Ni fedha ambazo wavuvi hao wamekuwa wakizisubiri kwa kipindi cha karibu miaka saba sasa.

Ikumbukwe kuwa mnamo Mei,2018, Mahakama Kuu mjini Malindi iliamuru jumla ya wavuvi wa Lamu 4,734 kufidiwa kima cha Sh1.76 bilioni.

Hii ni baada ya mahakama kupata kuwa mradi wa bandari ya Lamu ni kweli ulisababisha athari kubwa, ikiwemo kuharibu maeneo ambayo tangu jadi yalikuwa yakitegemewa na wavuvi hao wa Lamu kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Aidha idadi ya wavuvi hao ilipunguzwa hadi 4,125 baada ya Mamlaka ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) mnamo Aprili,2023 kuingilia kati na kutekeleza ukaguzi na kuamuru orodha mpya ya wavuvi halisi waliofaa kufidiwa iandaliwe.

Hatua hiyo ilitokana na kuwepo kwa tetesi kwamba shughuli ya uteuzi wa wavuvi halali walioathiriwa na mradi wa bandari ilizingirwa na ufisadi.

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumanne, Mwenyekiti wa Miungano ya Wavuvi wa Lamu (BMUs), Bw Mohamed Somo, alithibitisha kuwa ni kweli serikali kupitia KPA ilikuwa imeanza kutekeleza zoezi la kuwafidia wavuvi waathiriwa wa Lapsset.

“Twashukuru kwamba kilio chetu cha muda mrefu hatimaye kwa sasa kimegeuka kuwa kicheko. Serikali kuu kupitia KPA imeanza kutufidia. Fedha za fidia tayari zimeanza kuingizwa na kupokelewa kwenye akaunti za wavuvi wetu mbalimbali. Ni heko kwa serikali kutimiza ahadi ya fidia japo kuchelewa,” akasema Bw Somo.

Kaimu Afisa wa Mawasiliano na Uhusiano Mwema wa KPA, Jones Buchere pia alithibitisha kuwa ni kweli fedha za wavuvi waathiriwa wa Lapsset zimeanza kutolewa na kulipwa wanaofaa.

Kulingana na Bw Buchere, wavuvi 3,998 kati ya idadi ya jumla ya kwanza kabisa ambayo ni 4,734 tayari walikuwa wametumiwa fedha kwenye akaunti zao za benki mbalimbali kufikia Jumanne.

Bw Buchere aidha aliwataka wale ambao bado hawajafikiwa na fedha hizo kuwa watulivu wakati KPA ikiendelea kutekeleza zoezi hilo la fidia.

“Nataka kuthibitisha kwamba fedha za wavuvi zimetolewa na wameanza kuzipokea kwenye akaunti zao za benki. Tumetekeleza ukaguzi, kuhakiki na kupasisha wote wanaofaa kulipwa kupitia. Wote waliosalia katika ukaguzi na upasishaji wawe watulivu. Bado tunakuja na awamu nyingine ya ukaguzi, uhakikishaji na uidhinishaji ili kila mtu apate haki yake,” akasema Bw Buchere.

Kaimu Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Charles Kitheka pia alithibitisha kwamba serikali imetimiza ahadi yake ya kuwaipa wavuvi walioathiriwa na mradi wa Bandari ya Lamu.

Bw Kitheka aliwasihi wavuvi na jamii nzima ya Lamu kuendelea kushirikiana kwa karibu na serikali ili kuona kwamba maendeleo Zaidi yanafikishwa eneo hilo.

Pia aliwahakikishia wote waliosajiliwa kwenye orodha halali ya wanaofaa kulipwa kwamba watapokea fedha zao.

“Serikali kupitia KPA tayari inaendelea kuwalipa wavuvi wetu fidia zao kutokana na athari za ujenzi wa Bandari ya Lamu. Twatarajia kufikia mwishoni mwa juma hili kila mvuvi halisi aliyeandikishwa na kupasishwa apate haki yake. Wasiwe na shaka,” akasema Bw Kitheka.

Kulingana na maafikiano kati ya wavuvi waathiriwa, KPA, serikali kuu na ile ya kaunti, wavuvi watapokea asilimia 65 ya fidia hizo kama pesa taslimu ilhali asilimia 35 nyingine ikilipwa kwa mfumo wa vifaa vya kisasa vya uvuvi na uboreshaji wa miundomsingi mingine kwenye sekta hiyo ya uvuvi Lamu.

Kila mvuvi mnufaika binafsi anatarajiwa kupokea kima cha Sh241,700 kutoka kwa kitita hicho cha jumla ya Sh1.76 bilioni.

Malipo hayo yanatolewa wakati ambapo baadhi ya wavuvi tayari wamefariki wakati wakisubiri kulipwa fedha zao.

Kulingana na takwimu kutoka kwa ofisi ya miungano ya wavuvi (BMUs) kaunti ya Lamu, zaidi ya wavuvi 300 tayari wameaga kabla ya kuonja utamu wa hela hizo za fidia.