Habari MsetoSiasa

Fyata ulimi, Uhuru amuonya Kang'ata

August 3rd, 2020 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta Jumapili aliripotiwa kumuonya Kiranja wa Wengi katika Seneti, Irungu Kang’ata dhidi ya kutumia handisheki na BBI kusukuma kupitishwa kwa hoja ya mfumo mpya wa ugavi wa pesa za kaunti.

Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kuwa Rais Kenyatta hajafurahishwa na vitisho ambavyo Bw Kang’ata amekuwa akitoa kwa mrengo wa ODM kuwa Jubilee itavunja handisheki na BBI, iwapo maseneta wake hawataunga mkono mswada huo.

Habari zilisema Rais alimwambia Bw Kang’ata amwachie yeye binafsi na Kinara wa ODM Raila Odinga jukumu la kusaka idadi inayohitajika ya maseneta kupitisha mfumo huo mpya.

Baada ya mswada huo kupingwa na maseneta wengi Jumanne iliyopita, seneta huyo wa Murang’a alilaumiwa kuchangia hali hiyo kutoka na kauli yake ya vitisho.

Taifa Leo ilipompigia Bw Kang’ata simu alikiri kuagizwa na Rais kufyata ulimi: ‘Nimekuwa nikiongea na rais mara kwa mara, ndiposa nimeamua kukoma kutotoa matamshi yoyote hadharani kuhusu suala hili hadi litakapotatuliwa.’

Haya yalijiri huku Rais Kenyatta pia akimwagiza Waziri wa Fedha, Ukur Yatani kuandaa kikao cha dharura leo ili kubuni njia mbadala za kugawa pesa kwa kaunti kwa lengo la kuziwezesha kufadhili matumizi ya dharura kama mishahara na kupambana na janga la Covid-19 iwapo kesho Seneti itashindwa kusikizana.

Mkutano huo utashirikisha Spika wa Seneti Ken Lusaka, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya, Kinara wa wengi Seneti Samuel Phoghisio, Bw Kang’ata na mwenyekiti wa kamati kuhusu fedha katika CoG, Wycliffe Wangamati.

Mfumo huo mpya wa ugawaji fedha kwa kaunti umeungwa mkono na maseneta wanaowakilisha maeneo yenye idadi kubwa ya watu, huku wale wa yenye watu wachache wakipinga.

Upinzani mkubwa umetoka kaunti za Pwani, Kaskazini na Ukambani.Maseneta hao wanalalamika kuwa mfumo huo mpya utasababisha kupunguzwa kwa mgao wa pesa kwa kaunti zao.