Habari za Kitaifa

Gachagua aapa kuadhibu wanasiasa watundu Rift Valley

March 17th, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

NAIBU Rais, Rigathi Gachagua ameapa kukabiliana na wanasiasa ambao huleta aibu katika mikutano ya Rais William Ruto kutoka jamii ya Wakalenjin.

Bw Gachagua aliambia wanasiasa husika na viongozi wengine kutoka jamii ya Wakalenjin na nchi kwa jumla kujiepusha na siasa za kutupiana cheche za maneno mbele ya Rais na kuleta aibu.

Bw Gachaugua aliapa kukabiliana na wanasiasa hao kama alivyofanya wanasiasa wa Mlima Kenya.

Naibu wa Rais alisema kuwa ni jambo la aibu na kukosa heshima kwa wanasiasa kutoka jamii ya Wakalenjin kuonyesha uozo wao wa kisiasa mbele ya Rais Ruto wakati wa shughuli za umma.

Akirejelea kisa cha hivi majuzi huko Kericho ambapo kambi mbili zinazozozana wakati wa hafla ya Rais, Bw Gachagua alisema kitendo hicho kinaonyesha ukosefu wa heshima kwa afisi ya rais.

“Nilichoona Kericho kilikuwa ni dhihaka kubwa na ukosefu wa heshima kwa rais. Tabia kama hiyo lazima ikomeshwe, ilikuwa ni aibu kubwa hadharani,” akasema Bw Gacahgua.

Bw Gachagua ameahidi kuitisha mkutano wa viongozi wote kutoka Jamii ya Wakalenjin aliowashutumu kwa kukosa heshima.

Naibu Rais ambaye alionekana kuwa na hasira dhidi ya viongozi waliohusika na tukio la Kericho alisema kuwa yuko tayari kuadhibu wanasiasa hao kama alivyofanya katika eneo la Mlima Kenya.

“Mlimani tulikuwa na kelele za aina hiyo lakini niliadhibu viongozi waliokuwa na tabia hiyo mbaya na niko tayari kufanya vivyo hivyo kwa viongozi kutoka jamii ya Wakalenjin na hivi karibuni nitawaita katika mkutano wa nidhamu,” alisema Bw Gachagua.

“Jinsi nilivyosimama kidete nyumbani kwangu Mlima Kenya kwa kuwashinda viongozi waliokuwa wakileta aibu mbele ya Rais Ruto, nitaleta mjeledi huo hapa. Niliwaambia kuwa Rais ni Rais wa Kenya na lazima wakome utovu wa nidhamu mbele yake na wakakoma. Ninawahimiza viongozi kutoka jamii ya Wakalenjin kumheshimu Rais wetu,” akasema Bw Gachaugua.

Alisema inasikitisha kuwa Rais Ruto anaheshimiwa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla, ilhali watu wake nyumbani wanamdharau.

“Rais wetu anaheshimika Afrika Mashariki na ukanda mzima ilhali hapa nyumbani tunamkosea heshima, hivi karibuni nitawaita viongozi hao kwenye mkutano ili niwatie adabu,” akasema Bw Gachagua.

Viongozi waliokuwepo wakati wa hafla hiyo walimpongeza Bw Gachagua kutokana na juhudi zake katika vita vyake vya dhati dhidi ya pombe haramu.