Gachagua aendeleza kauli za kukanganya

Gachagua aendeleza kauli za kukanganya

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameendelea kuteleza kwenye matamshi yake, hali ambayo imezilazimu taasisi muhimu za serikali kukanusha kauli zake ama kujitenga nazo.

Kauli hizo za Bw Gachagua zimeibua maswali, kwani baadhi zinakinzana na sera na msimamo wa serikali mpya ya Rais William Ruto.

Hapo Jumapili, iliilazimu Benki Kuu ya Kenya (CBK) kukanusha madai ya Bw Gachagua, kwamba Kenya inakumbwa na uhaba wa fedha za kigeni kiasi cha kukosa fedha za kutosha za kigeni kuagiza mafuta.

“Tunakabiliwa na uhaba wa fedha za kigeni kutokana na kuingiliwa na maafisa wa serikali iliyopita. Maafisa hao walikuwa wakimiliki benki zilizokuwa zikitoa huduma za ubadilishanaji wa fedha hizo. CBK haikuwa na udhibiti wowote wa ubadilishanaji wa fedha hizo,” akasema Bw Gachagua, kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha Citizen.

“Jumamosi ilitulazimu kufanya mkutano wa dharura kwani CBK haina fedha za kigeni za kutosha kutuwezesha kununua mafuta.”

Hata hivyo, benki hiyo ilikanusha madai ya Bw Gachagua, ikisema kuwa Kenya ina fedha za kutosha za kigeni kuiwezesha kuagiza bidhaa tofauti kwa miezi minne ijayo.

Kwenye taarifa, CBK ilisema huwa haitoi fedha za kigeni kwa mashirika au matumizi ya kibinafsi, bali kwa Serikali ya Kitaifa pekee, ili kuiwezesha kuagiza bidhaa na kulipa madeni ya kimataifa.

Benki hiyo ilifafanua kuwa kuwa wafanyabiashara kama vile waagizaji mafuta huwa wanapata fedha hizo kutoka kwa benki za kawaida: “Waagizaji mafuta huwa wanapata fedha za kigeni kutoka kwa benki za kawaida wala si kutoka kwetu.”

Kauli hiyo ya kukanganya ya Bw Gachagua imejiri siku chache tu baada ya Bw Gachagua kuteleza tena kuhusu mpango wa serikali kuwaruhusu Wakenya kuanza kulima kwenye misitu.

Jumamosi iliyopita, wakati wa mazishi ya aliyekuwa Naibu Gavana wa Baringo, Bw Charles Kipng’ok, Bw Gachagua aliahidi serikali ya Kenya Kwanza itarejesha mfumo ambapo wananchi walikuwa wakiruhusiwa kulima katika misitu.

Mfumo huo ulikosolewa vikali na wanamazingira maarufu nchini, na pia unaikinzana na manifesto ya Kenya Kwanza ambayo inaahidi kujitolea kuhifadhi mazingira.

Kauli nyingine ilikuwa ni kufusu mfumo wa elimu a CBC, ambapo Rais William Ruto na Bw Gachagua walisema wangeufutilia mbali kwa msingi kuwa ukitekelezwa bila kuwashirikisha Wakenya wote.

Hata hivyo, walibadilisha msimamo wao baada ya Rais Ruto kuteua jopokazi la zaidi ya watu 49 kutathmini masuala tata katika mfumo huo.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti kutoa ardhi zaidi kwa ajili ya upanzi wa kahawa

Mung’aro aacha kanisa gizani kuhusu hospitali

T L