Siasa

Gachagua agusa kaa moto la ‘mtu mmoja, shilingi moja’

May 28th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua anaendelea kukumbana na vita vikali kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya kuhusu kauli yake ya kuunga mkono mfumo wa kugawa rasilimali kwa kuzingatia idadi ya watu.

Huku akiwa na uungwaji mkono kutoka kwa wanasiasa wa mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya wa kutoka eneo hilo, mbunge wa Laikipia Mashariki Bw Mwangi Kiunjuri anamuona Bw Gachagua kama mnafiki.

“Mfumo huo unaweza ukaletwa kupitia uamuzi wa Baraza la Mawaziri, sheria Bungeni au refaranda ya kikatiba lakini sio kupitia mikutano ya kisiasa jinsi anavyofanya Bw Gachagua,” akasema Bw Kiunjuri.

Alimtaka Bw Gachagua aelewe kwamba akiwa ni mmoja wa wale ambao hushiriki mikutano ya Baraza la Mawaziri, anafaa kusukuma ajenda hiyo hapo Rais William Ruto akiwa badala ya kutoa tamko la aina hiyo katika mikutano ya kisiasa.

Kwa upande wake, Bw Gachagua amewasuta wale ambao hupinga mfumo huo kuwa wasaliti wa kijamii.

Tayari, Bw Gachagua amesema wananchi wanafaa kuwa makini sana na wawatumbue wasaliti wa jamii za Mlima Kenya ambao wanapinga.

Mshauri wa Rais Ruto kuhusu masuala ya uchumi Bw David Ndii ni mwingine ambaye amepinga hadharani mfumo huo.

Bw Gachagua akihutubu akiwa katika eneo la Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga mnamo Mei 19, 2024, alisema kwamba yeyote anayepinga mfumo wa ugavi wa pesa kwa mujibu wa idadi ya watu ni msaliti.

Bw Gachagua alisema kwamba sawa na wafuasi wa mrengo wa Azimio katika ukanda wa Mlima Kenya, anaunga mkono mfumo huo.

Alikuwa akiongea katika eneo la Gichugu alipohudhuria mazishi ya mwalimu Julius Kano Ndumbi.

“Wanaopinga mfumo huo ni sawa na wale wasaliti waliokuwa wakihujumu vita vya ukombozi vya Maumau,” akasema Bw Gachagua.

Bw Ndii ni mzawa wa Kaunti ya Kiambu na ni wa jamii ya Agikuyu.

Hata hivyo, Bw Ndii katika chapisho katika ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa X na pia katika chapisho la maoni ya usomi, alikariri kwamba wanaotetea mfumo huo ni waliokwama katika fikra za ubinafsi.

Alisema kwamba wengi Mlima Kenya wamezama katika mwonekanio wa ubinafsi kiasi kwamba wanatamani kudhibiti rasilimali za kitaifa bila kujali walio katika maeneo ambayo yametengwa kwa muda mrefu.

Bw Ndii alisema kwamba mfumo huo haufai kuzingatiwa kama sera ya kitaifa kwa kuwa utapendelea maeneo yaliyo na utajiri wa jadi, udongo ulio na rutuba, na yaliyo na miundombinu bora inayofanya maendeleo kuafikiwa kwa wepesi.

Bw Ndii alisema kwamba mfumo huo ni wa kutenganisha, kudhulumu, kubagua na kudunisha walio katika maeneo yaliyotengwa kwa muda mrefu.

Lakini Bw Gachagua alisema kwamba “hao tumewazoea na tutaishi nao jinsi walivyo”.

“Lakini furaha yangu ni kwamba, kati ya wasaliti 10, huwa tuko na wazalendo na mashujaa 1 milioni,” akasema Bw Gachagua.

Wengine walio ndani ya serikali ambao wameelezea shaka yao kuhusu ufaafu wa mfumo huo ni pamoja na Seneta wa Nyandarua Bw Kaba Methu na Mbunge wa Kangema Bw Peter Kihungi.