Gachagua aibuka bingwa wa kuteleza

Gachagua aibuka bingwa wa kuteleza

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amegeuka kuwa bingwa wa kukanganya sera na ahadi za utawala mpya, wiki mbili pekee tangu alipoapishwa.

Ijapokuwa lengo kuu la semi zake ni kuendeleza umaarufu wa serikali mpya ya Kenya Kwanza, nyingi zimeibuka kuwa kinyume na ahadi zilizotolewa na mrengo huo wakati wa kampeni.

Mnamo Jumamosi wakati wa mazishi ya aliyekuwa Naibu Gavana wa Baringo, Bw Charles Kipng’ok, Bw Gachagua aliahidi kuwa serikali ya Kenya Kwanza itarejesha mfumo tata wa kulima kwenye msitu, maarufu kama “shamba system”.

“Ni kinaya kuwa tunaagiza chakula kutoka mataifa ya nje ilhali tunawazuia wananchi kulima katika misitu. Tutawaruhusu kufanya hivyo baada ya kumteua waziri wa mazingira afaaye,” akasema Bw Gachagua.

Mfumo huo ulisimamishwa na serikali ya Mwai Kibaki, ukilaumiwa kuchangia ukataji miti na uharibifu wa misitu.

Mfumo huo pia ulikosolewa vikali na wanamazingira maarufu nchini, akiwemo marehemu Profesa Wangari Mathai, aliyeshinda Tuzo ya Nobeli mnamo 2005, kutokana na juhudi zake katika utetezi na uhifadhi wa mazingira.

Kwenye manifesto ya Kenya Kwanza, Rais Ruto na Bw Gachagua waliahidi kufanya kila wawezalo kuendeleza uhifadhi wa mazingira.

Kwenye hotuba yake katika Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York, Amerika wiki iliyopita, moja ya masuala aliyoangazia pakubwa Rais Ruto ni athari za mabadiliko ya hali ya hewa nchini Kenya na Upembe wa Afrika.

Kando na hayo, alichaguliwa kuongoza mkutano maalum wa viongozi wa Afrika katika kongamano hilo kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Wadadisi wanataja kauli ya Bw Gachagua kuhusu kuruhusu kilimo katika misitu kuwa kinyume na juhudi za serikali hiyo kuendeleza uhifadhi wa mazingira.

KAULI KUPINGWA

“Naiunga mkono serikali ya Kenya Kwanza katika ajenda zake zote. Hata hivyo, kwa hili ninapinga kabisa; suala la kulima msituni,” akasema wakili Ahmednassir Abdullahi.

Wakati wa kampeni zao, wawili hao walisema kuwa wangefutilia mbali Mfumo Mpya wa Elimu (CBC), wakishikilia umekuwa ukitekelezwa bila kuwashirikisha Wakenya wote.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Rais Ruto alisema atabuni jopo la wataalamu kutoa ushauri kuhusu mfumo huo na hatua zinazopasa kuchukuliwa.

Lakini akiongea jijini Kisumu wiki iliyopita, Bw Gachagua alikanusha kulikuwa na mpango wa kufutilia mbali CBC, akisisitiza badala yake wataufanyia mabadiliko ili kuuboresha.

Siku chache baada ya kuapishwa, Bw Gachagua aliteleza alipoelekezea kidole cha lawama Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), ambayo wakuu wa Kenya Kwanza walikosoa wakati wa kampeni kwa madai ya kuwahangaisha.

Hii ni licha ya Rais William Ruto kuahidi kuwa hawatalipiza kisasi dhidi ya walioonekana kutumiwa kuhujumu safari yao ya kwenda Ikulu.

“Lazima maafisa wa DCI wangoje makosa kuripotiwa katika makao yao, wala si kukaa katika afisi za serikali wakiwahangaisha viongozi waliochaguliwa. DCI ianze kuwaheshimu viongozi,” akasema Bw Gachagua.

Kulingana na Profesa Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, kuna uwezekano kauli hizo zikawa kikwazo kwa Kenya Kwanza kutimiza baadhi ya ahadi zao.

“Huenda baadhi ya kauli hizi zikawa kikwazo kwa utekelezaji wa ahadi hizi, kwani zinapaswa kuwiana na ahadi walizotoa. Wanafaa waanze kutathmini athari zake na jinsi zinavyochukuliwa na raia, kwani baadhi wataanza kuwaona kama waongo na vigeugeu,” akasema Prof Macharia kwenye mahojiano na Taifa Leo jana Jumatatu.

Wakili Miguna Miguna naye alimshauri Bw Gachagua kuepuka matamshi yasiyozingatia sera za serikali.

  • Tags

You can share this post!

Maasi dhidi ya Putin yachacha maelfu wakitoroka Urusi

Wales wateremshwa ngazi kwenye Nations League baada ya...

T L